1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robben akiri "kupiga mbizi", aomba radhi

30 Juni 2014

Huwa siyo jambo la kawaida kwamba mchezaji anaweza kujitokeza hadharani na kuungama kwamba alipiga mbizi ili kutafuta penalti katika mchezo, lakini hivyo ndivyo alivyofanya mshambuliaji wa Uholanzi Arjen Robben

https://p.dw.com/p/1CSmc
WM 2014 Achtelfinale Niederlande
Picha: Reuters

Laana ya duru ya mchujo kwa vijana wa Mexico katika Kombe la Dunia bado haijavunjwa kabisa. Huku wakicheza katika raundi ya pili kwa mara ya sita mfululizo katika dimba hilo, Wamexico walionekana ni kama hatimaye wamefanya sawa kila kitu walichohitaji kukifanya dhidi ya Uholanzi

Ulinzi wao imara ulikuwa umeyazuia mashambulizi ya Waholanzi, huku mlinda lango Guillermo Ochoa akiokoa makombora motomoto. Wamexico walipata goli kupitia kwa Giorvani Dos Santos katika kipindi cha kwanza baada ya kufanya shambulizi baada ya jingine katika lango la vijana wa Louis Van Gaal. Na hata refarii akausimamisha mchuano huo mara mbili angalau wachezaji waweze kukata kiu kutokana na joto kali mjini Fortaleza.

WM 2014 Achtelfinale Niederlande Fan
Ilikuwa ni uchungu kwa mashabiki wa Mexico baada ya ndoto yao kukatizwa ghafla na UholanziPicha: Getty Images

Na katika dakika ya 88, Ochoa hangeweza kuzuia shuti kali ya Wesley Sneijder aliyefanya mambo kuwa moja moja. Dakika chache baadaye, Klaas Jan Huntelaar aliwafungia Waholanzi bao la ushindi kupitia penalty katika dakika za majeruhi, baada ya Arjen Robben kuangushwa na Rafael Marquez. Kocha wa Mexico Miguel Herrera amelalamika sana kwamba penalty hiyo ilikuwa ya kubuniwa tu. Robben akizungumza baada ya mechi, alikiri kuwa ni kweli alipiga mbizi mara kadhaa katika kipindi cha kwanza, na jambo hilo limemsikitisha sana. Ameomba radhi kuhusiana na tabia hiyo, na lakini amesisitiza kuwa penalty yake iliyowapa ushindi ilikuwa halali. Huyu hapa Robben

Uholanzi sasa watapambana Jumamosi mjini Salvadore na Costa Rica ambao waliwashangaza wengi kwa kuwabandua nje Ugiriki katika mechi ambayo iliamuliwa na mikwaju ya penalti. Vijana hao wa Amerika ya kati walicheza kwa kujituma licha ya kuwa walikuwa wamechoka sana kutokana na kibarua walichokifanya cha kulinda lango lao baada ya kiungo Oscar Duarte kutimuliwa uwanjani.

Mechi hiyo ilikamilika kwa sare ya goli moja kwa moja katika muda wa kawaida na wa ziada. Costa Rica walifunga penalty zao zote tano, kabla ya kuokolewa na shujaa wao mlinda lango Keylor Navas aliyezuia penalty moja ya Ugiriki.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AP/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman