1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rishi Sunak kutawazwa rasmi waziri mkuu Uingereza

25 Oktoba 2022

Mfalme Charles wa Tatu kumkabidhi Sunak majukumu ya kuunda serikali mpya

https://p.dw.com/p/4IeIb
UK Premierminister Rishi Sunak
Picha: Stefan Rousseau/empics/picture alliance

Nchini Uingereza Rishi Sunak anatwaa rasmi  uongozi wa nchi baada ya kuchaguliwa jana  kurithi nafasi iliyoachwa na waziri mkuu aliyejiuzulu Liz Truss.Hii leo Sunak atapewa rasmi majukumu ya kuunda serikali na mfalme Charles wa tatu.

Maandalizi yameshuhudiwa yakiendelea leo asubuhi katika mtaa wa Downing Street iliko ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza, kwa ajili ya kumpokea waziri mkuu mpya Rishi Sunak.

Liz Truss aliyejiuzulu anamkabidhi madaraka mrithi wake huyo baada ya kujiuzulu wiki iliyopita kufuatia siku 45 za misukosuko akiwa anaiongoza Uingereza.

Großbritannien 10 Downing Street
Picha: Daniel Leal/AFP

Bwana Sunak anakuwa waziri mkuu wa tatu tangu mwezi Septemba na waziri mkuu wa kwanza mwenye asili ya Asia nchini Uingereza.

Waziri mkuu huyu mpya na baraza lake la mawaziri atakaowateua watalazimika kukabiliana na migogoro iliyopo ya kiuchumi na kisiasa na kupatia majibu ya haraka.

Waziri mkuu anayeondoka Liz Truss ametowa tamko lake la mwisho kwa umma nje ya ofisi ya Downing Street kabla ya kuachia  rasmi madaraka hii leo ikiwa ni wiki saba  baada ya kuteuliwa waziri mkuu na hayati Malkia Elizabeth wa pili.

Miongoni mwa aliyoyasema ni pamoja na kuwa na imani kwamba waingereza wanapaswa kupunguziwa mzigo wa kodi lakini pia Ukraine haipaswi kuachwa peke yake katika mapambano na Urusi.

''Hivi  sasa ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote tunapaswa kuwaunga mkono Ukraine katika mapambano yao ya ujasiri dhdi ya uchokozi wa Putin.Ukraine lazima ishinde na tunapaswa kuendelea kuimarisha mifumo yetu ya ulinzi na hilo ndilo nililokuwa nataka kulifikia.Na namtakia Rishi Sunak mafanikio kwa ajili ya nchi yetu.''

Bildergalerie | Liz Truss
Picha: Hannah McKayREUTERS

Mfalme Charles wa Tatu amesimamia jukumu la kupokea barua ya kujiuzulu Truss katika kasri la Buckingham kabla ya kumpa idhini Sunak ya kuunda serikali.

Sunak alichaguliwa kukiongoza chama chama cha Conservative jana Jumatatu wakati chama hicho kikijaribu kuuimarisha uchumi na umaarufu wake ndani ya Uingereza ambao umeporomoka kufuatia kipindi kifupi cha janga chini ya uongozi wa Liz Truss.

Sunak mwenye umri wa miaka 42 anakuwa waziri mkuu mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kutokea Uingereza kwa kipindi cha miaka 200 iliyopita na muhimu zaidi atalazimika kujaribu kuukoa uchumi wa Uingereza na kuiépusha nchi hiyo kuingia kwenye mporomoko mkubwa wa kiuchumi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW