Risala za pongezi zamiminika mjini Berlin
28 Septemba 2009Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, atakaeendelea na wadhifa wake kwa mara ya pili kufuatia uchaguzi mkuu wa jana, amesema anapendelea kuunda serikali mpya hadi ifikapo November 9 ijayo,Ujerumani itakaposherehekea miaka 20 ya kuporomoka ukuta wa Berlin. Risala za pongezi zinazidi kumiminika kutoka kila pembe ya dunia.
Katika mkutano pamoja na waandishi habari hii leo mjini Berlin, kansela Angela Merkel amesema angependelea pamoja na serikali mpya, kuwakaribisha viongozi kadhaa wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya na wageni wengineo, katika sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya kuporomoka Ukuta wa Berlin.
Amekumbusha bunge jipya la shirikisho litakutana October 27 ijayo, kama ilivyotajwa katika katiba ya shirikisho la jamahuri ya Ujerumani.
Kansela Angela Merkel ameendelea kusema:
"Tunataka kuharakisha. Bila ya shaka tunatanguliza mbele ubora .Lakini ninaamini Ujerumani inastahiki kupata serikali mpya haraka, kwa sababu tumeendesha kampeni za uchaguzi kwa miezi kadhaa- tuna majukumu chungu nzima mbele yetu na tunabidi pia tuhakikishe kwamba Ujerumani inajipatia pia serikali mpya haraka."
Katika wakati ambapo Ujerumani inaisubiri kwa hamu serikali mpya ya muungano kati ya vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU na waliberali wa FDP, risala za pongezi zinazidi kumiminika katika ofisi ya kansela mjini Berlin.
Wa mwanzo kutuma risala za pongezi alikua rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy. Rais wa Ufaransa, aliyemuombea kansela Merkel "kila la kheri na ufanisi kwa mhula wa pili wa miaka minne," ameelezea matumaini yake ya kuona tunanukuu "uhusiano wa aina pekee kati ya nchi zao mbili" ukizidi kunawiri." Mwisho wa kumnukuu rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy.
Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu jana kansela Angela Merkel kumpongeza kwa ushindi wake. Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Marekani, rais Barack Obama ameelezea matumini ya kuiona serikali imara ya Ujerumani ikiimarisha na kuzidisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
"Marekani na Ujerumani ni washirika wawili wa dhati na wanashirikiana katika kuimarisha uhuru, usalama na neema ulimwenguni," amesema rais Obama katika risala yake ya pongezi kwa kansela Angela Merkel.
Rais Obama ameelezea furaha yake ya kuendelea kushirikiana na kansela Angela Merkel ili kukabiliana na changamoto zijazo."
Risala kama hizo za pongezi zimetolewa pia na kiongozi wa serikali ya Italy, Silvio Berlusconi, anaesema ushindi wa kansela Angela Merke katika uchaguzi mkuu ni ushindi wa familia nzima ya wahafidhina barani Ulaya."
Nchini Ujerumani kwenyewe, mashirika ya kiuchumi yamempongeza pia kansela na kusisitiza ushindi wa wahafidhina na waliberali utazidi kuinua shughuli za kiuchumi nchini Ujerumani.
"Ni kura bayana kwa ajili ya mageuzi ya kijasiri"-amesema mwenyekiti wa shirikisho la mashirika ya viwanda na biashara, DIHK- Hans Heinrich Driftman hii leo mjini Berlin.
"Serikali ya muungano wa nyeusi na manjano inaweza kuiokoa Ujerumani na mgogoro wa kiuchumi."Amesisitiza mwenyekiti huyo wa shirikisho la mashirika ya viwanda na biashara DIHK.
Mwandishi Hamidou Oumilkheir(DPA/Afp
Mhariri:Othman Miraji