1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN-Afghanistan

Sekione Kitojo31 Julai 2009

Umoja wa mataifa umetoa ripoti yake kuhusu hali ya mambo nchini Afghanistan ukisema kuwa mapigano yanasababisha raia wengi kuuwawa.

https://p.dw.com/p/J14k
Mwakilishi maalum wa Marekani kwa ajili ya Afghanistan na Pakistan Richard Holbrooke, kulia, akizungumza na waziri wa mambo ya kigeni wa jamhuri ya Czech Helena Bambasova.Picha: AP


►Umoja wa mataifa umetoa ripoti yake leo kuhusu hali ya mambo nchini Afghanistan ukisema mapigano nchini humo yanasambaa katika maeneo wanamoishi raia ambako watu wengi wanauawa kutokana na mashambulio ya ndege, mabomu ya kutegwa garini na mashambulio ya kujitoa mhanga.


Afisi ya umoja wa mataifa ya misaada kwa Afghanistan imesema kwamba raia 1,013 waliuawa katika mapigano nchini mwao kuanzia Januari hadi Juni ikilinganishwa na 818 katika nusu ya mwaka 2008 na 684 katika kipindi hicho hicho mnamo 2007.



Akizungumzia ripoti hiyo, Kamishna mkuu wa umoja wa mataifa anayehusika na haki za binaadamu Bibi Navi Pillay alisema ni muhimu zichukuliwe hatua kuwalinda raia na jamii kutokana na mapigano.


Bibi Pillay ambaye ni raia wa Afrika kusini, alisema pande zote zinazohusika katika mgogoro wa Afghanistan zinapaswa kuchukua hatua za kuwalinda raia na kuhakikisha kunaendeshwa uchunguzi wa visa vyote vya mauaji ya raia wasio na hatia na kuwahakikisha haki inapatikana ikiwa ni pamoja na kuwalipa fidia wahanga.


Wapiganaji wa Taliban na washirika wao wametajwa kuwa wanabeba dhamana ya 59 asili mia ya mauaji ya raia wasio na hatia, hasa kutokana na mirpuko inayotengwa kandoni mwa barabara. Majeshi ya Afghanistan na yale ya kimataifa nayo yamelaumiwa kwa mauaji kutokana na hujuma zinazofanywa na ndege za kivita zilizoasababisha vifo vya mamia ya raia.


Ripoti inasema majeshi ya Afghanistan ya kimataifa yameendesha harakati zao katika maeneo ambako wanaishi waafghan wa kawaida, wakiwauwa watu na kuharibu nyumba na mali zao na pia miundo mbinu.

Umoja wa mataifa umeonya kwamba upinzani dhidi ya kuongezeka kawa idadi ya wanajeshi wa Marekani na juhudi za kuvuruga uchaguzi wa mwezi ujao wa Agosti, ni mambo yanayoweza kusababisha kupotea kwa maisha ya waafghan wengi zaidi.


Idadi ya raia waliuwawa katika ripoti hiyo ya umoja wa mataifa inatokana na maelezo ya mashahidi na mahojiano na maafisa wa kijeshi na viongozi katika maeneo husika nchini Afghanistan, ziara hospitalini pamoja na filamu na picha za ushahidi na ripoti za vyombo vya habari.


Ripoti hii ya karibuni imesema raia 200 wameuwawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu katika hujuma 49 za ndege zilizofanywa na majeshi yanayoiunga mkono serikali . Mwezi Mei ndiyo ulikua wa umwagaji damu zaidi, wakiuwawa raia 63 katika hujuma moja ya anga na jumla ya raia 81 katika kipindi hicho.

Ripoti hiyo imetolewa wakati mjumbe maalum wa Marekani kwa Afghanistan Richard Holbrooke akisisitiza ju ya ushirikiano zaidi wa majeshi ya kimataifa na serikali ya Afghanistan kuliko ilivyokua kabla.

Ripoti imegundua kwamba ingawa kwa wakati huu idadi ya mashambulio ya ndege za kiviata inaweza kuwa imepungua lakini yanapotokea huangamiza maisha ya watu wengi. pia imegundua kwamba kuna visa ambapo matumizi ya nguvu ya kupindulikia yaliofanywa na wanajeshi wa Aghanistan na wale wa kimataifa pia yamesababisha vifo pasina sababu yoyote.


Mwandishi: Sekione Kitojo / Reuters

Mhariri: M. Abdul-Rahman