1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya shirika la kimataifa la kupambana na njaa duniani

29 Juni 2012

Juhudi za kupambana na njaa,madai ya waasi wa M23 kusaidiwa na mashariki ya Kongo na madai kama mabwana wa kivita wa kisomali wanashirikiana na Mafia nchini Italy ni miongoni mwa mada magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/15O65
Mwenyekiti wa shirika la kimataifa la kupambana na njaa Bärbel DieckmannPicha: dapd

Tuanzie lakini na gazeti la Neues Deutschland linaloelezea kuhusu ripoti ya mwaka 2011 ya shirika la kimataifa la kupambana na njaa-inayoitaja kinga kuwa ndio mikakati muhimu ya kupambana na njaa.Baada ya kuzungumzia juhudi zinazoendeshwa tangu miaka 50 iliyopita na shirika hilo la kimataifa katika nchi nyingi za dunia ili kuimarisha hali ya chakula,Neues Deutschland linasema kuna baadhi ya hatua zilizofanikiwa ingawa bado njia ni ndefu .Mnamo mwaka 1962 asili mia 30 ya wakaazi wa dunia walikuwa wakisumbuliwa na njaa, idadi hiyo imepungua hivi sasa na kusalia asili mia 13.

Gazeti la Neues Deutschland limemnukuu mwenyekiti wa shirika hilo la kimataifa la kupambana na njaa Bärbel Dieckmann akisema idadi hiyo ni kubwa ukitambuliwa ukweli kwamba asili mia 13 ni sawa na wakaazi milioni 925 wa dunia.

Bibi Bärbel Dickmann amesema hali hiyo haikubaliki ukizingatiwa ukweli kwamba duniani kuna chakula cha kutosha kuweza kuwatosha watu bilioni saba.Mwenyekiti huyo wa shirika la kimataifa la kupambana na njaa,amelitaja balaa la njaa katika kambi kubwa kabisa ya wakimbizi ulimwenguni huko Dedaab-wanakoishi watu laki tano waliokimbia ukame na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.

Gazeti la Neues Deutschland limemnukuu mwanasiasa huyo wa chama cha Social Democratic ,meya wa zamani wa Bonn,Bärbel Dickmann akihimiza upatikane ufumbuzi wa kisiasa ili njaa itoweke ulimwenguni.

Kongo Rebellen
Waasi katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasi ya KongoPicha: picture-alliance/dpa

Tuhuma kwamba Rwanda inawasaidia waasi wa M23 mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo zimeripotiwa na gazeti la Die Tageszeitung la mjini Berlin.Wanaotafutwa zaidi kujiunga na kundi hilo jipya la waasi Mashariki ya jamhurim ya kidemokrasi ya Kongo ni wale wanamgambo wa zamani wa kihutu wa FDLR. Ripota wa gazeti la Die Tageszeitung akiwa Goma na Gisenyi anazungumzia kisa cha vijana 24 wa kirwanda wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 21.Tangu april mwaka huu vijana hao wanajikuta ndani ya kambi ya muda wa Umoja wa mataifa iliyozungushwa senyenge huko Goma.Vijana hao wanadai ni wahutu na wameandikishwa walipokuwa vijijini mwao nchini Rwanda ili kama wanavyosema,kujiunga na kundi jipya la waasi la M23 linaloongozwa na majenerali wa kitutsi.Wametoroka tena na kukimbilia katika kikosi cha Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo mjini Goma.Vijana hao sasa wamegeuka kuwa mashahidi wa madai ya kuhusika Rwanda katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kongo.Wapiganaji wengine wa kutoka Rwanda wanashikiliwa na wanajeshi wa serikali ya Kongo,gazeti la Die Tageszeitung linaandika.Rwanda inakanusha madai hayo lakini .Gazeti linasema serikali ya Kongo inawatuhumu baadhi ya wanachama wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuzuwia kuchapishwa ripoti ya utafiti ya Umoja huo inayotoa ushahidi wa kuhusika Rwanda na vita vya Mashariki ya Kongo.

Somalia Anti-Pirateneinsatz Atalanta
Helikopta ya kikosi cha kimataifa cha kupambana na maharamia wa kisomali-AtalantaPicha: AP

Na hatimae lilikuwa jarida la Der Spiegel lililoandika kuhusu uchunguzi unaofanywa na Umoja wa Ulaya kuhusu madai kwamba mabwana wa kivita wa Somalia wanayasaidia makundi ya Mafia ya Italy.Katika ripoti yake jarida la Der Spiegel linazungumzia kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili ili kwa upande mmoja maharamia wa kisomalia wapatiwe silaha na badala yake wakuu wa kivita wayaruhusu makundi ya Mafia ya Camorra na Ndrangheta wamwage takataka zao za sumu katika fukwe za Somalia katika bahari ya Hindi.Madai hayo yanachunguzwa hivi sasa,amenukuliwa mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya kwa pembe ya Afrika Alexander Rondos.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman