Ripoti ya mkuu wa vikosi vya NATO na Marekani nchini Afghanistan
1 Septemba 2009Ripoti ya kiongozi mpya wa vikosi vya Marekani na jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO nchini Afghanistan,Stanley McChrystal,imezusha patashika mjini Washington.Anashauri mkakati mzima wa kijeshi ubadilishwe nchini Afghanistan.Kinachohitajika zaidi ni mshikamano na ushirikiano imara-kipa umbele kikiwa hifadhi ya raia-amesema Stanley McChrystal katika ripoti hiyo ambayo haizungumzii juu ya kuzidishwa idadi ya wanajeshi.
Ikulu ya Marekani mjini Washington haijasema lolote kwasasa kuhusu ripoti hiyo.Msemaji wa ikulu ya Marekani Robert Gibbs anasema wanasubiri kwanza ripoti ya komanda wa vikosi vya jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO nchini Afghanistan,Stanley McChrystal iwasilishwe rasmi mjini Washington.Hapo ndipo watakapoipima na kuwataka wataalam waidurusu.Hata hivyo kimoja ni bayana:
"Patahitajika vyenzo zaidi ambavyo rais alikwisha ahidi vitatolewa.Kwa miaka sasa kumekua na uhaba wa fedha ,vifaa na wanajeshi kusimamia vita vya Afghanistan."
Hadio mwisho wa mwaka huu rais Barack Obama aliahidi kutuma wanajeshi 6000 zaidi kujiunga na 62 elfu walioko nchini Afghanistan.Maoni ya wananchi lakini yanapinga fikra hiyo.Utafiti wa maoni ya umma uliochapishwa wiki iliyopita umedhihirisha takriban nusu ya wakaazi wa Marekani wanapendelea idadi ya wanajeshi wao nchini Afghanistan ipunguzwe.Na kwa mara ya kwanza tangu vita vya Afghanistan viliporipuka,idadi kubwa ya wamarekani wanahisi vita hivyo havina maana yoyote kwa nchi yao.
Wanajeshi 47 wameangukia mhanga wa vita hivyo mwezi uliopita,idadi kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika miaka minane ya vita vya Afghanistan.Hata hivyo msemaji wa ikulu ya Marekani Robert Gibbs anaamini wanaweza kuwashinda maadui.
Wanajeshi laki moja wa NATO wanakutikana nchini Afghanistan.Thuluthi mbili ya wanajeshi hao ni wa kutoka Marekani .Jenerali McChrystal anahisi idadi hiyo ni ndogo. Bado si rasmi kama ripoti ya jenerali Stanley McChrystal inazitaka pia nchi shirika na hasa Ujerumani zichangie wanajeshi zaidi au la nchini Afghanistan.
Hata hivyo jenerali Egon Ramms anaeshughulikia harakati za vikosi vya pamoja vya jumuia ya kujihami ya NATO huko Brunssum na hivyo kusimamia moja kwa moja shughuli za vikosi shirika nchini Afghanistan anasema:
"Kwa maoni yangu panahitajika vikosi zaidi,kuliko wale walioko.Kwa upande wa Ujerumani,nnadhani wakati umewadia wa kutafakari kwa namna gani tunaweza kusaidia ili kuhakikisha ushindi katika eneo hilo."
Itafaa kusema hapa kwamba Ujerumani imetuma wanajeshi 4300 nchini Afghanistan na inapanga kutuma wanajeshi 200 zaidi.Wanajeshi wa Ujerumani wanakutikana katika eneo la kaskazini la Afghanistan.
Ripoti ya jenerali Stanley McChrystal inasemekana inazungumzia mkakati wa aina mpya wa namna ya kuendesha vita nchini Afghanistan,mada ambayo rais Barack Obama ameitaja kua kipa umbele cha siasa ya nje ya nchi yake.
Mwandishi Paulert,Rüdiger (NDR/WDR) Hamidou Oummilkhheir
Mhariri:Abdul Rahman