Ripoti ya Amnesty International dhidi ya mahabusu, Iraq.
13 Septemba 2010Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu la Amnesty International lenye makaazi yake mjini London linakadiria kuwa watu elfu 30,000 wanashikiliwa katika magereza ya Iraq, huku wengine kadhaa wakifa wakiwa vizuizini.
Mkurugenzi wa shirika hilo, katika kanda ya Mashariki kati na Afrika kaskazini Malcolm Smart amesema majeshi ya Iraq yamekuwa yakiwajibika kwa uvunjifu wa haki za mahabusu na kwamba wamekuwa wakiruhusiwa kufanya hivyo bila ya kuadhibiwa.
Amesema mamlaka nchini Iraq zinapaswa kuchukua hatua za dhahiri sasa, kuonesha nia yake ya kisiasa kuruhusu haki za binadamu kwa Wairaq wote, kulingana na sheria ya kimataifa pamoja na kukomesha vitendo vya mateso na unyanyasaji mwengine yanayokwenda kinyume na haki za watu hao waliko vizuizini.
Katika ripoti yake yenye kurasa zipatazo 59, yenye kichwa cha habari ''Mfumo mpya, Unyanyasaji ule ule'', shirika hilo limeorodhesha idadi ya wanaume kadhaa ambao wameteswa ama wamekufa wakiwa mahabusu.
Miongoni mwa hao ni Riad Mohammed Saleh al Oqaibi , ambaye alikamatwa Septemba mwaka 2009 na kuwekwa kizuizini mjini Baghdad kabla ya kuhamishwa katika kizuizi cha siri katika mji huohuo wa Baghdad.
Katika maelezo yake yaliyomo katika ripoti hiyo al Oqaibi, inasemekana wakati alipokuwa akihojiwa, alikuwa akipigwa sana kifuani na kwamba mbavu zake zilivunjiak na ini kuharibika. Alikufa Februari 12 ama 13 mwaka huu kutokana na kuvuja damu kwa ndani.
Kulingana na shirika hilo la Amnesty, njia zinazotumiwa kutesa watu hao ni pamoja na nyanya za umeme, mabomba ya mpira, kuvunja viungo, kumtesa mtu kisaikolojia kama vile kumtishia kutaka kumbaka pamoja na mateso mengine makali.
Aidha inasemekana kuwa majeshi ya usalama katika jimbo lenye utawala wake wa ndani la Kurdstan pia ni wakulaamiwa, kwa kutolea mfano kesi moja ambapo mahabusu mmoja alikuwa akishikiliwa kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kufunguliwa mashtaka au kuhukumuwa na inadaiwa alikuwa akiteswa na polisi wa Kikurd.
Shirika la haki za binadamu la Amnest International linasem pia kwamba katika kipindi cha mwezi wa Aprili wanaume wa Kiiraq walibakwa, kuuawa kwa umeme na kupigwa katika magereza ya siri mjini Baghdad, hali iliyofanya wabunge kutaka kufanyika kwa uchunguzi huru juu ya vitendo vya unyanyasaji magerezani.
Tangu kuanzia mwezi wa saba mwaka huu Iraq imechukua majukumu kamili ya kuongoza magereza nchini humo, huku Marekani ikiwajibika katika kitengo kidogo cha mahabusu katika gereza la Karkh nje ya mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad.
Katika sherehe za za kukabidhiwa udhibiti wa mahabusu ya mwisho iliyokuwa ikishikiliwa na Marekani Julai 15, waziri wa sheria wa Iraq Dara Nureddine Dara alisema siku za kuwanyanyasa na kuwatendea vibaya wafungwa zimekwisha na kwamba watamchunguza na kumchukulia hatua mtu yoyote anatayebainika kufanya makosa.
Shirika la Kimataifa la Amnesty International limeitaka serikali ya Iraq kuwalinda vyema wafungwa.
Halima Nyanza(afp)
Mhariri:Abdul-Rahman