Ripoti: Watu milioni 55 walikimbilia ndani ya nchi zao 2020
20 Mei 2021Shirika linalofuatilia watu walioachwa bila makaazi katika nchi zao limetoa ripoti yake hii leo inayoonesha kwamba vita na majanga, yanayosababishwa mara nyingi na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi, vimewalazimu watu kuyahama makaazi yao, ndani ya nchi zao zaidi ya mara milioni 40, mwaka uliopita.
Ripoti ya shirika hilo la mjini Geneva, la kufuatilia wakimbizi wa ndani ya nchi zao inasema watu milioni 55 hawaishi kwenye makaazi yao lakini wapo ndani ya nchi zao. Na rikodi hiyo ni ya kufikia mwishoni mwa mwaka jana, kutokana na hali ya vimbunga na mafuriko iliyoshuhudiwa pamoja na vita na migogoro mipya.
Matukio hayo yameonekana kuiongeza idadi ya wakimbizi wa ndani ambayo imekuwa ikiongezeka kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja. Imeelezwa kwenye ripoti hiyo kwamba wakati mwingine watu wamelazimika kuhamamara mbili au hata tatu.
Shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva, Uswisi ambalo ni sehemu ya baraza linaloshughulikia masuala ya wakimbizi la Norway, limesema idadi ya watu walioachwa bila makaazi ndani ya nchi zao ni kubwa zaidi ya mara mbili ya idadi ya wakimbizi kutoka nje,kwa mujibu wa takwimu za kufikia mwishoni mwa mwaka jana.
Shirika hilo limetahadharisha kwamba inawezekana idadi hiyo ni ndogo kuliko hali halisi ilivyo kwasababu vizuizi vya usafiri katika kipindi cha janga la Covid-19 vimesababisha changamoto katika ukusanyaji wa data. Jan Egeland, katibu mkuu wa baraza la kushughulikia masuala ya wakimbizi la Norway NRC, amesema inashtusha kuona kwamba mtu analazimika kukimbia makaazi yake akiwa ndani ya nchi yake, katika kipindi cha kila sekunde moja, mwaka jana.
Amesema ulimwengu unashindwa kuwalinda watu walioko kwenye hatari kubwa duniani kutokana na migogoro na majanga.
Hali ilivyo
Inaelezwa katika ripoti hiyo kwamba kati ya watu walioachwa bila makaazi ndani ya nchi zao kufikia mwishoni mwa mwaka,kiasi milioni 48 walikimbia vita na machafuko na milioni 7 wengine walikimbia majanga.
Migogoro iliyochangia hali hiyo iliyotajwa na Shirika hilo la mjini Geneva ni vita vilivyosambaa na harakati za makundi ya itikadi kali katika nchi kama Ethiopia, Msumbiji na Burkina Faso mwaka jana na vita vinavyoendelea katika nchi nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Syria na Afghanistan.
Kadhalika limesema mamilioni ya watu wameachwa bila makaazi kutokana na majanga makubwa ya vimbunga vya msimu katika maeneo ya Amerika, Asia na eneo la Pasifiki na misimu ya mvua za muda mrefu katika mashariki ya kati na kusini mwa jangwa la Sahara.
Kwa ujumla idadi kubwa ya watu walioachwa bila makaazi ndani ya nchi zao mwaka jana imeshuhudiwa China ambako mafuriko yanashuhudiwa mara kwa mara na maafisa wakiwahimiza wakimbizi hao wa ndani kuondoka kwenye maeneo ya mafuriko. Ufilipino na Bangladesh nazo zinafuatia. Zaidi ya watu milioni 5 huko China walilazimika kuyaacha makaazi yao na kubakia bila sehemu ya kuishi mwaka jana.