Ripoti: Vifo vinanvyosababishwa na UKIMWI vyapungua
16 Julai 2019Katika ripoti yake ya kila mwaka, Umoja wa Mataifa umesema vifo vinavyosababishwa na maradhi ya UKIMWI vilipungua kwa takriban vifo 770,000. Idadi hiyo inawwakilisha asilimia 33 ya vifo vilivyotokea mnamo mwaka 2010 ambapo watu milioni 1.2 walikufa. Hata hivyo katika ripoti yake Umoja wa Mataifa umesema maambukizi yameongezeka katika Mashariki ya Kati na Ulaya Mashariki.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeitaka jumuiya ya kimataifa iweke mkazo katika juhudi za kuyakabili maradhi hayo. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo watu wapatao milioni 37.9 wanaishi na virusi vya UKIMWI duniani. Watu milioni 23.3 wenye virusi hivyo wanapata dawa za kudhibiti maambukizi. Hata hivyo bado pana hali ya wasiwasi.
Umoja wa Mataifa umesema licha ya hatua hiyo ya mafanikio iliyopigwa, juhudi za kuutokomeza ugonjwa huo zimelegalega kutokana na ufadhili wa fedha wa kiwango cha chini na pia kutokana na watu walio katika baadhi ya maeneo kutopata huduma muhimu za afya.
Katika ripoti yake Umoja wa Mataifa umesema idadi ya vifo imepungua kwa kiwango kikubwa katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, ingawa mikasa ya maambukizi bado ni mingi.Hata hivyo vifo kutokana na UKIMWI vimeongezeka kwa asilimia 5 katika nchi za Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Ulaya Mashariki.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI Gunilla Carlsson ametoa mwito wa kuwepo dhamira ya kisiasa katika juhudi za kupambana na maradhi hayo. Amesema dhamira ya kisiasa ni muhimu katika juhudi za kuwasaidia watu walio katika maeneo yaliyoachwa nyuma.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa maambukizi yameongezeka miongoni mwa watu wasiopata huduma za kuepusha maambukizi hayo lakini pia Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa fedha zinazohitajika kwa ajili ya kutoa huduma za kupambana na maradhi ya UKIMWI zimepungua. Mwaka jana kiasi cha fedha kilichotolewa kilikuwa dola bilioni 19 yaani pungufu ya dola bilioni 7, kiasi kinachohitajika hadi kufikia mwakani ni dola bilioni 26.2.
Chanzo: https://p.dw.com/p/3M8YZ