1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa yazinduliwa Berlin

13 Aprili 2014

Jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi hatimae limetoa ripoti yake mpya mjini Berlin Jumapili ikigusia juu ya tafauti baina ya malengo ya kimataifa kupambana na kuongozeka kwa ujoto duniani.

https://p.dw.com/p/1BhEK
Athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Athari za mabadiliko ya tabia nchi.Picha: picture-alliance/dpa/Oliver Berg

Jopo hilo limesema kwamba utoaji wa gesi chafu ya carbon dioxide na nyengine zinazochafua mazingira lazima upunguwe kwa asili mia 40 hadi 70 ifikapo 2050, ili kulifanya ongezeko la joto kuwa chini ya digrii mbili za nyuzi joto, kiwango kilichowekwa katika mikutano ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa . Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya iliotokana na majadiliano ya wiki nzima,kwa wastani utoaji wa gesi zinazochafua mazingira duniani umeongezeka kwa gigatani 1 kwa mwaka baina ya mwaka 2000 na 2010 na hivyo ongezeko jumla miongo iliiopita kufikia viwango visivyotarajiwa .

Licha ya juhudi za kujaribu kuzuwia hali hiyo. Mmoja wa wenyeviti watatu wa jopo hilo linalotathmini njia za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi Ottmar Edenhofer ni kwamba , kuna ujumbe ulio wazi nao ni kwamba , ili kuepusha hatari ya kujiingiza katika mifumo ya tabia nchi, tunahitaji kujitoa katika ile dhana ya kuendelea na shughuli kama kawaida .

Jopo hilo la kiserikali, halikuzingatia suala la nani afanye nini katika ufupisho wa ripoti yake ya kurasa 33 ambayo imekusudiwa itumiwe kama muongozo wa kisayansi kwa serikali zilizo kwenye mashauriano kuhusu mkataba mpya wa mazingira, unaotarajiwa kupitishwa mwaka ujao.

Mswaada wa waraka huo, unaonyesha sababu kuu ya kuongezeka uchafuzi wa mazingira kutokana na gesi chafu ni mahitaji makubwa ya nishati yanayotokana na ongezeko la idadi ya watu hasa nchini China na katika nchi nyengine kubwa..

Akizungumzia ripoti hiyo mkurugenzi wa sera ya nishati wa fuko la maumbile duniani Stephen Singer amesema,“ Bila shaka kungali na pengo fulani katika baadhi ya utendaji kuhusu nishati mbadala. Hapana shaka katika baadhi ya mambo nishati mbadala hazipunguzi gharama kama ambavyo ingepaswa iwe, lakini tusisahau nishati zilizopo zimeiendesha sayari hii kwa miaka 150 iliopita na bado zina pata sehemu kubwa ya uwekezaji na fidia.”

Ukame na athari nyengine za mazingira zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa uchumi, kilimo na afya ya binaadamu hasa katika nchi zinazoendelea.

Kufuatia ripoti hiyo mpya ya Umoja wa Mataifa, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema mjini Washington kuwa hiyo ni fursa kwa dunia na kuongeza kusema kwamba teknolojia nyingi mpya zitakazoisaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ni rahisi, zinaweza kupatikana kwa urahisi zaidi na ni bora zaidi kiutendaji, ikilinganishwa na zile zilizokuweko pale ripoti ya mwisho ya jopo hilo ilipotolewa takriban mwongo mmoja uliopita.

Akaitaja ripoti hiyo kuwa sio tu ni ukumbusho wa kitisho kinachotokana na mabadiliko ya tabia nchi, bali pia tija zinazoweza kupatikana hasa katika sekta ya nishati , kutokana na kuzuwiwa kwa mabadiliko hayo.

Baada ya siku sita za vuta nikuvute, Jumamosi Serikali ya Ujerumani iliidhinisha ripoti hiyo ya Umoja wa mataifa ilioorodhesha mapendekezo mbadala kuweza kupunguza gesi zinazosababisha uharibu wa mazingira. Ripoti hiyo ilioandaliwa na zaidi ya wanasayansi 200 katika kipindi cha miaka mine, ni ya tatu kuhusiana na mtazamo jumla wa jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (IPCC)

Generalsekretärin des Sekretariats der Klimarahmenkonvention der Vereinten Nationen Christiana Figueres
Picha: picture-alliance/AP Photo

Ripoti mpya inagusia mengi ikiwa ni pamoja na faida za kiuchumi, zitakazotokana na kupungua kwa ongezeko la joto duniani. Mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa anayesimamia mazungumzo kuhusu mkataba mpya wa kupunguza viwango vya gesi zinazochafua mazingira Christiana Figueres ameyataka mataifa kuongeza kasi ya uwajibikaji wa pamoja.

Waraka wa mjini Berlin uliopitiwa kifungu kwa kifungu na wajumbe pia umeonya, kwa mwenendo huu wa sasa, dunia itakuwa na ongezeko zaidi la joto katika kiwango ambacho wanasayansi wanasema kinaweza kuwa janga.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp,ap

Mhariri:Mohamed Dahman