1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti kuhusu waislamu nchini Marekani yatolewa

23 Mei 2007

Licha ya kutopendwa sera za mambo ya nje za Marekani pamoja na rais wake George W Bush, waislamu nchini humo wana utulivu na wanaridhika na idadi kubwa ya jamii hiyo inayo ishi nchini Marekani kuliko wenzao wanaoishi katika maeneo ya bara ulaya.

https://p.dw.com/p/CHkq
Waislamu nchini Marekani
Waislamu nchini MarekaniPicha: AP

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika la uchunguzi la Pew la nchini Marekani.

Takriban watu elfu 60 walishiriki katika uchunguzi huo kwa kuhojiwa na matokeo yalionyesha kuwa vijana wa kiisalmu wenye umri kati ya miaka 18 hadi 29 wanajiweka karibu zaidi na dini yao na pia wanaunga mkono vitendo vya kujitoa muhanga na mashambulio kuliko vijana wa dini zingine.

Lakini mawazo kama hayo yamepungua sana kwa vijana wa kiislamu wa nchini Marekani ukilinganisha na nchi kama Ufaransa, Uhispania na Uingereza na pia ukilinganisha na matokeo ya uchunguzi wa mwaka mmoja uliopita.

Uchunguzi huo mpya pia umebaini kuwa ni idadi ndogo tu ya waislamu wa nchini Marekani ambao wanaamini kuwa maisha yao yamekuwa magumu tangu yalipotokea mashambulio ya Septemba 11, mwaka 2001 au pia kunyanyaswa kutokana na imani yao ya dini ya kiislamu.

Thuluthi mbili kati ya hao wamesema kuwa wamepata pongezi na hata kutambuliwa kwa juhudi zao makazini hata ingawa wao ni waislamu na hivyo basi wamethibitisha kuwa maisha yao ni mazuri na wana mahusiano mazuri na Wamarekani wenzao.

Uchunguzi huu ni wa kina kuwahi kufanyika kuhusu waislamu nchini Marekani.

Shirika la Pew limesema kuwa takriban waislamu milioni 2.35 ni raia wa Marekani, asilimia 24 ni wa asili ya Kiarabu, asilimia 18 kutoka kusini mwa Asia, asilimia 8 kutoka Iran, wengine ni kutoka bara Uropa, nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara na sehemu zingine.

Asilimia 35 iliyobakia ni wazaliwa wa Marekani ambao ni Wamarekani weusi.

Uchunguzi huo umebaini kuwa asilimia 21 ya waislamu wazaliwa wa Marekani ni wale waliosilimu.

Waislamu wazaliwa wa Marekani pia wamesema kuwa hawaridhishwi na hali yao ya kifedha.

Robo tatu ya Waislamu waliohojiwa wamesema kuwa haikuwa jambo la busara kwa Marekani kuanzisha vita nchini Irak huku asilimia 48 wakisema kuwa ni makosa makubwa pia kwa Marekani kushiriki katika vita vya Afhganistan.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya hivi karibuni asilimia 11 ya waislamu nchini Marekani wanakiunga mkono chama cha Republican kinyume na asilimia 63 ya waislamu wanaokiunga mkono chama cha Demokratik.

Lakini waislamu wa Marekani wengi wao hawaiweki mbele fikra ya kuwa wao ni waislamu kabla ya utaifa wao tafauti na silimia 81 ya waislamu wa Uingereza,asilimia 66 nchini Ujerumani na asilimia 69 waislamu wa kutoka nchini Uhispania ambao kwanza wanajitangamanisha na dini yao kabla ya utaifa wao.

Kwa jumla uchunguzi huo umebaini kwamba waislamu nchini Marekani wanaabudu dini yao sawa na wakristo kwa kuzingatia kwenda miskitini sawa na wakristo wanaokwenda makanisani.

Kwa upande wa kisiasa waislamu nchini Marekani wanaunga mkono kutenganishwa dini na siasa tafauti na waumini wa kikristo, pia wengi wao wanapinga usilamu wenye msimamo mkali.