Ripoti kuhusu umaskini yachapishwa
19 Septemba 2012Tuanzie lakini na ripoti kuhusu hali ya umaskini katika jamii nchini Ujerumani.Gazeti la "Berliner Morgenpost" linaandika:
Ripoti mpya kuhusu matajiri na maskini miongoni mwa jamii nchini Ujerumani( yenye kichwa cha maneno cha kutisha na kusababisha husda),inatoa picha ya pengo linalozidi kuwa pana kati ya wanaopokea mishahara mikubwa mikubwa na wale ambao wanajikuta katika hali duni.Mshikamano miongoni mwa jamii huanza kuyumba yumba ikiwa hakuna daraja inayowaunganisdha wanaolipwa mishahara ya chini,mishahara ya wastani na wale wanaolipwa mishahara mikubwa mikubwa.Ikiwa tofauti ya mshahara miongoni mwa raia wa kawaida haiingii akilini na kufika hadi ya kuangaliwa kana kwamba imekithiri au si ya haki.Salama ya Mungu bado Ujerumani haijafikia daraja hiyo.Tatizo nchini humu linakutikana kati ya wanaolipwa mishahara ya wastani na wale wenye mishahara ya chini.
Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:Ujerumani ni miongoni mwa nchi tajiri.Lakini ugawaji wa utajiri huo si mzuri.Kwa wanasiasa.Kwa wenye kujiweza.Makosa unaweza kusema yanakutikana kwa kila raia ambae "hafanyi bidii" ya kumaliza masomo.Makosa lakini mtu anaweza kuwatwika watunga sheria wanaowatoza kodi kubwa zaidi wafanyakazi kazi kuliko wawekezaji.Ni kawaida lakini kuona ripoti kama hii ikizusha mijadala moto moto,mijadala ambayo haikawii kufifia.Kwa vyovyote vile kuna tofauti ikilinganishwa na epo ya matajiri nchini Marekani:Huku hakuna mwanasiasa mwenye daraja ya Mitt Romney anaesubutu kuwakashifu wasiolipa kodi na kuwaita "matapeli".Angalao kwasasa,bado hakuna.
Kumhusu mgombea huyo huyo wa kiti cha rais wa Marekani,Mitt Romney na matamshi yake makali,linaandika gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" Mitt Romney anajulikana kwa matamshi yake ya ufidhuli.Haya aliyoyatoa hivi karibuni yanaweza kuyamwaagia mchanga matumaini yake ya kisiasa.Matamshi makali kama hayo dhidi ya wapiga kura yanatosha kusababisha kupigwa kumbo mgombea yeyote yule.Katika kadhia ya Romney,matamshi hayo yamethibitisha zile dhana dhidi ya tajiri huyo mwenye dharau na kujinata.Romney,hawezi,na hatoweza kamwe kuwa rais wa raia wote wa Marekani.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/inlandspresse
Mhariri-Yusuf Saumu