Ripoti kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa yatolewa leo
2 Februari 2007Ripoti iliyoandaliwa na jopo la IPCC ni ya kwanza katika kipindi cha miaka sita na inajumulisha kazi iliyofanywa na maelfu ya wataalamu wa sayansi ulimwenguni kote. Duru mjini Paris Ufaransa zinasema maofisa wakuu wa jopo hilo wameitoa ripoti hiyo baada ya siku nne za mazungumzo. Binadamu analaumiwa kwa kusababisha asilimia 90 ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani na hali hii huenda isiweze kukomeshwa kwa karne nyingi zijazo.
Wanaharakati wa mazingira wamesema ripoti hiyo inatoa mwito wa haraka kukomesha matumizi ya gesi inayotokana na takataka zinazomeza miale ya joto la jua na kuendeleza ongezeko la joto duniani. Jan Kowalzig wa shirika la Marafiki wa Dunia barani Ulaya, amesema ripoti ya jopo la IPCC inatisha na inathibitisha kiwango cha janga lililolosababishwa na binadamu ambalo tayari linawaathiri watu wote duniani.
Sven Teske wa shirika la kimataifa la Greenpeace anasema hatua za haraka zinatakiwa zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
´Kimsingi tunaangalia janga kubwa. Tunaangalia hatari kubwa dhidi ya uchumi, tunaangalia mabadiliko makubwa katika hali yetu ya kimaisha kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika karne moja ijayo au zaidi. Kwa hiyo lazima tubadilike. Hatuwezi tu kupuuza ukweli wa mambo uliopo. Ukweli upo na lazima tuchukue hatua za kukabiliana na hali ilivyo hivi sasa.´
Ripoti hiyo pia inatoa tathmini ya mambo yatakayotokea katika siku za usoni ikiwa ni pamoja na vimbunga vikali, ukame na ongezeko la viwango vya maji baharini. Hatuwezi kuendelea kupuuza ilani zinazotolewa na wataalamu wa sayansi, ameongeza kusema Jan Kowalzig wa shirika la Friends of the Earth. Shirika hilo limesema dunia inakabiliwa na janga kubwa na limezitaka serikali zipunguze viwango vya gesi za viwandani.
Rais Jacques Chirac wa Ufaransa anakutana na wajumbe kutoka mataifa 60 katika ikulu yake leo asubuhi huku Ufaransa ikitaka hatua zichukuliwe kuyalinda mazingira. Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Baroso, anahudhuria mkutano huo. Rais Jacque Chirac amesema, ´Ulimwengu umeathiriwa na tabia ya kutumia malighafi kupita kiasi. Mwenendo huu unaibadili hali ya hewa na kuwaweka binadamu katika hatari, kama hatutachukua hatari za haraka.´
Shirika la kimataifa la kuyalinda mazingira, WWF, limesema serikali zinatakiwa kuhakikisha mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya hali ya hewa utakaofanyika mjini Bali Indonesia mwezi Disemba mwaka huu, unafanikiwa. Kiongozi wa shirika hilo anayehusika na mabadiliko ya hali ya hewa, Hans Verolme, amesema mkutano huo unatakiwa kuweka muda wa kufikia makubaliano ya kupunguza gesi kwa mujibu wa mkataba wa Kyoto yatakayoendeleza uwekezaji ambao hautakuwa na athari kwa mazingira.
Mkataba wa Kyoto ndio mkataba pekee wa kimataifa unaoweka viwango vya kupunguza uchafuzi wa mazingira kupitia gesi inayosababisha ongezeko la joto duniani. Mkataba huo umekataliwa na Marekani.