Ripoti iliyovuja: Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani
6 Juni 2017Shirika la Upelelezi la Marekani FBI limemkamata Reality Leigh Winner mwenye umri wa miaka 25, akiwa nyumbani kwake mjini Augusta jimbo la Georgia siku ya Jumamosi kulingana na taarifa za jana za Idara ya Sheria ya Marekani DOJ.
Winner anadaiwa kukiri kuchapisha taarifa za siri na kuzituma katika chombo kimoja cha habari mnamo mwezi Mei, kulingana na hati ya kiapo. Akikutikana na hatia anaweza kutumikia kifungo cha miaka kumi jela.
Winner alianza kufanya kazi katika Shirika la Usalama wa Taifa NSA mwezi Febuari na alikuwa na ruhusa ya kuzifikia nyaraka za siri za Marekani.
Naibu Mwanasheria Mkuu Jenerali Rod Rosenstein amesema watu walioaminiwa na kuapa kuzilinda siri za Marekani lazima wawajibishwe pale wanapokiuka jukumu hilo. "Kuvujisha nyaraka za siri ni kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi," ameongeza Rod Rosenstein.
Inasemekana kwamba watu sita walichapisha ripoti hiyo ya siri lakini, ni mtu mmoja tu - ambaye ni Winner- aliyekuwa na mawasiliano kwa njia ya barua pepe na chombo hicho cha habari kulingana na hati hiyo ya kiapo.
Chombo cha habari hakikutajwa
Pamoja na kwamba maafisa wa FBI walikataa kukitaja chombo hicho cha habari kilichopokea nyaraka hiyo ya siri, kukamatwa kwa Winner kulitangazwa saa moja baada ya tovuti ya habari ya The Intercept kuichapisha nyaraka hiyo ya siri kutoka Shirika la Usalama wa Taifa NSA inayoelezea jinsi majasusi wa jeshi la Urusi walivyoilenga programu ya kompyuta ya kupigia kura nchini Marekani ili kuweza kuiba data zake wakati wa uchaguzi nchini humo.
Alipoulizwa kuhusu kukamtwa huo kwa Winner, msemaji mkuu wa tovuti ya Intercept Vivian Siu amesema nyaraka ya NSA iliwafikia kupitia mtu asiyejulikana. Siu amesema tovuti ya Intercept haina taarifa zozote juu ya utambulisho wa chanzo cha nyaraka hiyo ya siri.
FBI pamoja na kamati mbalimbali sasa zitachunguza uwezekano wa kwamba wadukuzi wa Urusi pamoja na serikali ya Urusi waliingilia kati uchaguzi wa rais wa mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kuwepo uhusiano wowote kati ya timu ya kampeni za uchaguzi za Rais wa Marekani Donald Trump na maafisa wa Urusi.
James Comey kutoa ushahidi
Winner ni mtu wa kwanza kukamatwa juu ya kosa la kuvujisha taarifa za siri tokea Rais Donald Trump kuingia madarakani. Akiwa anakabiliwa na uvujaji wa baadhi ya sera zake, mazungumzo yake, na hasa juu ya uchunguzi wa uhusiano kati ya washauri wa kampeni yake na Urusi, Trump imewaaagiza maafisa wa Idara ya Sheria kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaovujisha siri za serikali ya Marekani.
Inaripotiwa kwamba Trump alimtaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi FBI James Comey kuanza kufikiria kuwakamata waandishi habari wanaochapisha taarifa za siri za serikali zilizovuja.
Alhamisi ijayo Comey –aliyeshangaza wengi wakati alipofutwa kazi na Donald Trump- atatoa ushahidi wake mbele ya Kamati ya Baraza la Seneti juu ya Urusi pamoja na uhusiano wake na rais Trump.
Mwandishi Yusra Buwayhid/dpae/afpe/dw
Mhariri: Caro Robi