Rio yajiandaa licha ya misukosuko
15 Aprili 2016Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro haitavurugwa na mchakato unaoendelea wa kutaka kumng'oa madarakani Rais wa Brazil Dilma Rousseff, kashfa ya rushwa ya dola biliomo 3 inayowahusu wanasiasa kadhaa maarufu pamoja na wafanyabiashara, na kuanguka uchumi wa nchi hiyo ambako hakujawahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa.
Huo ndio ujumbe uliotolewa na waandalizi wa Rio na wakaguzi wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC, ambao walikamilisha ziara yao rasmi ya maandalizi ya Rio ambapo michezo hiyo ya kwanza kabisa kuwahi kundaliwa Amerika ya Kusini iking'oa nanga chini ya miezi minne ijayo.
Nawal El Moutawakel, ni Mwenyekiti wa Tume ya mipango ya IOC kuhusu Rio 2016 "IOC ni shirika lisilo la kisiasa na tumekuwa tukiendelea na kazi yetu, licha ya mazingira magumu – ya kisiasa na kiuchumi. Na hii haiathiri Michezo kwa sababu itaandaliwa kwa wakati. IOC inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa muda wa mwisho unaheshimiwa na wakati kwa huu tuko mbele kuhusiana na operesheni nyingi. Na tunasubiri kesho kuona matokeo ya kura ya bunge dhidi ya rais".
Licha ya matumaini hayo, serikali ya Brazil inaonekana kuyumba huku kukiwa na vizuizi karibu na ofisi za seirkali mjini Brasilia kuwatenganisha waandamanaji wanaopinga na kuiunga mkono serikali wakati wabunge wakijiandaa kupiga kura kesho ya kuamua ikiwa Rousseff aondolewe madarakani au la.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Yusuf Saumu