1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice ajiengua kugombea uwaziri wa nje Marekani

14 Desemba 2012

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amejiengua katika kinyangányiro cha kuwania nafasi ya waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo kutokana na shutuma kutoka kwa wanasiasa wa chama cha Republican.

https://p.dw.com/p/172JS
Susan Rice
Susan RicePicha: Reuters

Rice amekuwa akikabiliwa na shutuma kali kutoka kwa wafuasi wa chama cha Republican kutokana na kauli aliyoitoa baada ya kutokea kwa mashambulizi dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, ambayo yalisababisha vifo vya maafisa wanne akiwemo Balozi Chris Stevens.

Rice, ambaye ni mshirika wa karibu sana wa Rais Barack Obama, amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani baada ya kiongozi wa sasa kwenye nafasi hiyo kutangaza kuwa hana mpango wa kuendelea na nafasi hiyo kwenye muhula wa pili wa utawala unaoanza mwakani.

Katika barua aliyomuandikia Rais Obama, Rice ameeleza kuwa anathamini heshima aliyompa ya kuwa mmoja kati ya watu wanaofikiriwa kwenye nafasi ya waziri wa mambo ya nje, lakini akasema kuwa anaamini kama atateuliwa, hatua hiyo inaweza kuambatana na mtafaruku wa kisiasa.

Rice amesema kuwa kuna mambo mengi ya muhimu utawala wa rais Obama umepanga kuyafanya kwa ajili ya wananchi hivyo hawezi kuhatarisha mafanikio ya mikakati hiyo kwa kung'ng'ania kuwa waziri wa mambo ya nje.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Kauli ya Rice kuwa mashambulizi ya Benghazi yalitokana na watu wenye hasira waliokuwa wakipinga filamu inayo mkashifu Mtume Muhammad wa dini ya kiislamu na si mashambulizi ya kigaidi ndiyo iliyomuweka katika kitimoto.

Rais Obama ametoa tamko kufuatia uamuzi huo akilaani kitendo cha kumsakama mama huyo kuwa hakikuwa cha kiungwana. Obama anasema hatua hiyo ni sawa na kumuonea Rice ambaye alitoa kauli hiyo kwa kuzingatia taarifa za kipelelezi alizopata kwa maafisa wa kijasusi wa nchi yake.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa sasa Rais Obama huenda akamgeukia Seneta John Kerry ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Marekani kutoka chama cha Democrat mwaka 2004 kuwa mtu mwenye nafasi zaidi ya kushika wadhifa huo.

Seneta John McCain.
Seneta John McCain.Picha: AP

Duru zinasema kuwa Obama atakuwa na kikao cha ndani na Bibi Rice katika ikulu ya White House baadaye hii leo. Rais Obama amesema kuwa Rice ataendelea na wadhifa wake kama balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.

Seneta John McCain wa chama cha Republican ambaye alipoteza kwenye mchakato wa kuwania urais wa Marekani mwaka 2008 dhidi ya Rais Obama ni mmoja kati ya wakosoaji wakubwa wa Rice. McCain ameapa kuendelea kuuchimba ukweli kuhusu mashambulizi ya Benghazi hadi hapo atakapoupata.

Mwandishi: Stumai George/AFPE/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel