Real Madrid yavunja rekodi yake ya uhamisho
2 Septemba 2013Nyota huyo wa Wales amekubali kujiunga na Real Madrid kwa kitita cha pauni za Uingereza milioni 85, sawa na euro milioni 100, kiasi ambacho ni zaidi ya pauni milioni 80, ambazo Real Madrid ililipa wakati inamsajili Chritiano Ronaldo mwaka 2009 kutoka Manchester United.
Bale alijiunga na Totenham Hotspurs kama beki wa kushoto mwaka 2007 akitokea klabu ya Southampton kwa kiasi cha pauni milioni 10, na alifunga magoli 26 msimu uliopita na kuchaguliwa kuwa mchezaji wa mwaka na chama cha wachezaji wa kulipwa na kile cha waandishi wa habari za soka.
Akizungumzia uhamisho wa Bale, Kocha wa Tottenham Hotspur Andre Villa Boaz alisema: "Ni mchezaji mzuri sana, anakwenda kujiunga na Real Madrid, kwa hiyo tunamtakia kila la kheri. Ametuachia kumbukumbu nzuri kutoka msimu uliopita, ambayo nadhani kila shabiki wa Tottenham anaiona. Lakini sasa ameamua kuendelea na sisi inatubidi tuendelee." Bale ametambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Real Madrid katika uwanja wa Barnabeu leo mchana.
Liverpool, Arsenal zashinda Uingereza
Katika michezo ya Ligi kuu ya Uingereza Premier Ligi mwishoni mwa wiki, Liverpool na Asenal zilipata ushindi wa goli moja kwa sifuri kila moja, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Manchester United na Tottenham Hotpurs siku ya Jumapili. Daniel Sturridge alifunga bao baada ya dakika nne katika uwanja wa Anfield katika siku ambayo klabu ya Liverpool ilikuwa ikisherehekea miaka100 ya kuzaliwa kwa meneja wake maarufu wa zamani Bill Shankly, matokeo ambayo yaliwapandisha hadi nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi wakiwa wameshinda mechi tatu.
Arsenal iliibuka mshindi dhidi ya wapinzani wao kutoka Kaskazini mwa London, Tottenham Hotspurs muda mfupi kabla ya kuthibitishwa kwa uhamisho wa Bale kwenda Real Madrid. Olivier Giroud aliweka wavuni goli pekee la Arsenal, na kama Sturridge, amefunga magoli matatu katika michezo mitatu msimu huu. Chelsea, ambao walipoteza kombe la Super Cup la Ulaya kwa Bayern Munich siku ya Ijumaa, wako katika nafasi ya pili, wakiwa nyuma ya Liverpool kwa pointi mbili, wakati Manchester City, ambao walishinda magoli 2-0 dhidi ya Hull City siku ya Jumamosi, Arsenal na Spurs wote wana pointi 6. Mabingwa Manchester United wana pointi 4.
Borrusia Dortmund yaendeleza ushindi
Henrikh Mkhitaryan alifunga magoli yake mawili ya kwanza ya Borrusia Dortmund tangu alipohamia katika klabu hiyo kwa kiticha cha euro milioni 27.5, na kuipa ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt, na hivyo kuendeleza rekodi yao ya asilimia 100 ya ushindi katika Bundesliga. VfB Stuttgart, ambao wameambulia vichapo katika mechi zao tatu za kwanza za Bundesliga, walifufuka kwa ushindi mnono wa magoli 6-2 dhidi ya Hoffenheim katika mchezo mwingine, wakihamasishwa na magoli matatu 'hat-trick' kutoka kwa mshambuliaji Vedad Ibisevic. Ushindi wa Dortmund uliwaacha wakishika usukani wa Bundesliga, wakiwa timu pekee yenye pointi 12 kutoka michezo yake minne ya kwanza. Mabingwa watetezi Bayern Munich, ambao walitoka sare na Freiburg siku ya Jumanne, wako pointi mbili nyuma katika nafasi ya pili, huku Hanover, Bayer Leverkusen na Mainz zikiwa na pointi 9 kila moja.
Lionell Messi atuma salamu kwa wapinzani
Katika La Liga ya Uhispania, Lionel Messi alipiga hat-trick ya tatu wakati Barcelona ikiendeleza mwanzo wake wa ushindi kutetea taji lake, katika ushindi wa kusisimua wa magoli 3-2 dhidi ya Valencia. Saa chache kabla ya kukamilisha uhamisho wa Gareth Bale kutoka Tottenham Hotspurs, Real Madrid ilipata ushindi wa tatu kutoka mechi tatu kwa kuifunga Atheltic Bilbao magoli 3-1 katika uwanja wa Bernabeu, na Athletico Madrid aliungana na magwiji hao wawili kwa pointi 9 kufuatia ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Real Sociedad.
Siku ya mwisho ya usajili
Wakati dirisha la uhamisho likiwa linafungwa leo Jumatatu, klabu ya Liverpool imefanikiwa kuwasajili mlinzi wa kimataifa wa Ufaransa Mamadou Sakho na beki wa kati wa Ureno Tiago Ilori, na kuwafanya wachezaji hao kuwa wa kwanza kuthibitishwa kuhamia katika ligi kuu ya Uingereza katika siku hiyo ya mwisho. Wachezaji hao wawili ambao waliishuhudia Liverpool ikishinda goli 1-0 dhidi ya Manchester United jana Jumapili, walisaini mikataba yao baada ya kukamilisha vipimo vya afya. Kuwasili kwa wachezaji hao kunamaanisha kocha wa Reds Brendan Rodgers amesajili jumla ya wachezaji saba wakati wa dirisha la usajili, wengine wakiwa Kolo Toure, Lago Aspas, Luis Alberto, Simon Mignolet na Aly Cissokho.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape, ap, afpe, rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo