1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid yatwaa ubingwa wa 11 wa Ulaya

29 Mei 2016

Cristiano Ronaldo alifunga penalti ya ushindi wakati Real Madrid waliwafunga watani wao Atletico Madrid kwa mara ya pili katika misimu mitatu katika fainali ya Champions League, mabao 5-3 kupitia penalti

https://p.dw.com/p/1IwZ4
Fußball Champions League Finale Atletico Madrid v Real Madrid
Picha: Reuters/C. Recine

Ronaldo alifunga mkwaju wake wa penalti baada ya Juanfran wa Atletico kushindwa kufunga wake na kuhakikisha kuwa Real wanashinda dimba hilo maarufu la kandanda barani Ulaya kwa mara ya 11 na kuivunja moyo Atleti kwa mara nyingine.

Mabao yalikuwa ni moja kwa moja baada ya dakika 90 na 120. Mchezaji bora wa fainali hiyo Sergio Ramos alifunga katika dakika ya 15, Atletico wakakosa kufunga penalti kupitia Antoine Griezmann mapema katika kipindi cha pili lakini mchezaji nguvu mpya Yannick Carrasco alisawazisha katika dakika ya 79.

“nilijua nitafunga, nilikuwa na uhakika wa hilo”, alisema Ronaldo. “nina furaha kubwa. Nilijuwa itakuwa fainali ngumu. Michuano hii huwa migumu”. Aliongeza.

Fußball Champions League Finale Atletico Madrid v Real Madrid Elfmeterschießen Ronaldo Jubel
Cristiano Ronaldo hakuwa na mchezo mzuri licha ya kufunga penalti ya ushindi ya Real MadridPicha: Reuters/C. Rellandini

Kocha wa Real Zinedine Zidane – ambaye alichukua usukani Januari – amekuwa kocha wa saba kunyakua kombe hilo la kifahari akiwa mchezaji na kocha. Mfaransa huyo anajiunga na kikundi cha Miguel Munoz, Giovanni Trapattoni, Johan Cruyff, Carlo Ancelotti, Frank Rijkaard na Pep Guardiola.

“Nna furaha kubwa, furaha kubwa kwa yote tuliyofanikisha pamoja”, alisema Zidande. “kwa sababu siyo rahisi kabisa kushinda Champions, tuliipigania”.

Atletico ndiyo klabu ya kwanza kushinda fainali tatu katika dimba hilo bila kuwahi kushinda kombe hilo. Walishindwa na Real miaka miwili iliyopita na Bayern Munich mwaka wa 1974. Timu ya Diego Simeone iliwabandua mabingwa watetezi Barcelona na Bayern katika duru zilizopita kabla ya fainali lakini Real ndiyo ilikuwa timu yenye bahati katika fainali hiyo uwanjani San Siro, Milan, Italia.

“Tulianza vibaya lakini tulikuwa na kitu kingine zaidi ndani yetu” alisema Simeone. “Katika kipindi cha pili tulikuwa na nafasi ya ksawazisha haraka sana. “pia nao walikuwa na kitu lakini tulifanikiwa kusawazisha. Ulikuwa mchezo wa mbinu zaidi, na wa kuchosha sana kwa timu zote mbili. Kwangu mimi, hakuna anayeikumbuka timu ya pili, timu iliyoshindwa. Tumeshindwa fainali mbili…na tunastahili kusahau hili na kuyauguza majeraha yetu”.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Mohammed Dahman