Real Madrid yasherehekea ubingwa wa Ulaya
5 Juni 2017
Ni shamra shamra zilizofana sana jana katika uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo maelfu ya mashabiki walikusanyika jana Jumapili kusherehekea pamoja na wachezaji wao taji la 12 ambalo limekuja baada ya kuishinda Juventus Turin siku ya Jumamosi mjini Cardiff , Wales kwa mabao 4-1 na kuwa timu ya kwanza katika bara la Ulaya kuweza kutetea taji hilo na kulinyakua kwa mara ya pili mfululizo.
Real madrid imekuwa timu ya kwanza kulibakisha kombe hilo katika kabati lao la mataji katika mfumo uliopanuliwa wa mashindano hayo , na kuonesha uwezo wake na nguvu zao dhidi ya timu nyingine zote barani Ulaya.
Kocha mkuu wa Real Madrid Zinedine Zidane ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa klabu hiyo kuweza kunyakua mataji mawili La Liga na Champions League katika msimu mmoja tangu mwaka 1958 baada ya kuzima kitisho cha Barcelona kuweza kunyakua taji la ligi ya Uhispania. Mshambuliaji mahiri wa timu hiyo Cristiano Ronaldo aliyefunga mabao mawili katika mchezo huo wa fainali alisema ulikuwa msimu wa kufurahisha sana.
"Moja, Mbili , Tatu ,(.....akishangiria....) shukrani nyingi kwa kuwapo hapa. Ukweli ni kwamba ulikuwa msimu mzuri sana. Ningependa kuwashukuru wachezaji wenzangu wooote, makocha wetu . Tuko hapa kusherehekea. Na shukrani kwenu nyie kwa kuendelea kutuunga mkono. Asanteni sana".
"Wachezaji wameingia katika kundi la wachezaji maarufu wa Real Madrid na soka, kama ilivyo kwa kocha wetu," amesema rais wa klabu hiyo Florentino Perez, wakati akitoa sifa maalum kwa Zinedine Zidane.
Zidane , ambaye ni Mfaransa , ambae binafsi alishinda taji hilo la Champions League akiwa mchezaji lejendari kwa Real kati ya mwaka 2001 na 2006, amepata mafanikio makubwa tangu kuingia katika jukumu lake hilo la juu kuiongoza timu hiyo miezi 18 iliyopita. Nae alisema.
"Tumekuwa na mwaka mzuri sana na nawashukuru nyie wote mashabiki kwasababu mlituamini tangu mwanzo na tumeweza kushinda mataji mawili."
Atmo: We are the champions.......
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / ape / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga