Real Madrid washerehekea ubingwa wao
28 Mei 2018Kwa mwaka wa tatu mfululizo Real Madrid walisherehekea taji lao la Ulaya la Champions League na mashabiki wao jana Jumapili. Madrid walirejea nchini Uhispania jana Jumapili wakitokea Ukraine walikolinyakua kombe hilo na walilitembeza katika mitaa ya jiji la Madrid wakati maelfu ya mashabiki wakifurahia na kuwashangiria mabingwa hao wapya.
Madrid walirejea nchini Uhispania baada ya kushinda taji lao la 13 la Ulaya kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya FC Liverpool mjini Kiev siku ya Jumamosi.
Sherehe hizo ziliishia katika uwanja wa Santiago bernabeu uliojaa mashabiki lukuki huku wachezaji na mashabiki wakipiga kelele Cristiano Ronaldo abakie katika klabu hiyo.
Hii ni kutokana na matamshi ya mshambuliaji huyo wa Real Madrid mara baada ya ushindi siku ya jumamosi na kuashiria katika mahojiano kwamba anatarajia kuondoka kutoka katika klabu hiyo. Alisema "ilikuwa furaha kubwa kuwapo Real Madrid".
Mreno huyo alionekana kuwa katika hali nzuri zaidi wakati wa sherehe hizo mjini Madrid na kuamsha matumaini ya mashabiki kwamba hataondoka kwa kusema "tuonane mwaka ujao".
Sherehe zilianza kwa wachezaji na viongozi wa timu kushiriki katika ibada katika kanisa la eneo karibu na klabu . Kisha walikutana na meya wa jiji na rais wa eneo hilo kabla ya kuzungumza na mashabiki kutoka katika dirisha katika uwanja wa Puerta del Sol, moja kati ya maeneo muhimu ya jiji la Madrid.
Katika mahojiano baada ya ushindi mchezaji wa kati wa Real Madrid raia wa Ujerumani Tony Kroos alizungumzia ushindi wa timu yake.
"Nafikiri katika kipindi cha kwanza tulianza kuizowea hali zaidi na zaidi. Tulichukua udhibiti wa mchezo na tulianza kucheza vizuri kabla ya nusu ya kwanza kwisha. Na tulianza kipindi cha pili kwa nguvu na kwa jumla nahisi tulistahili kuwa mabingwa."
Vitisho vya kuuwawa
Kwa upande wa Liverpool hali haikuwa shwari , kwani baada ya kuondoka uwanjani mshambuliaji wao tegemeo Mohamed Salah matumaini yalififia na pia kupata pigo la pili kwa makosa mawili makubwa ambayo hayana maelezo sahihi kutoka kwa mlinda mlango wa timu hiyo Loris Karius. Shabiki mmoja wa Liverpool Rob Middleton ambaye alisafiri kutoka New Zealand kuja kushuhudia pambano hilo mjini Kiev , hakuweza kuzuwia shutuma zake kwa Loris Karius.
Polisi nchini Uingereza itafanya uchunguzi wa vitisho vya kuuwa vilivyotolewa dhidi ya mlinda mlango huyo wa Liverpool Loris Karius baada ya mchezo huo wa Champions League. Karius alishambuliwa katika mitandao ya kijamii baada ya makosa yake mawili kuisaidia Real Madrid kushinda ubingwa wa Champions League, ambapo wengi walioandika walimuombea kifo Mjerumani huyo na famialia yake.
"Nina maana ,ni bahati mbaya kile alichofanya jioni ya leo lakini nafikiri utakuwa mchezo wake wa mwisho kwa Liverpool leo. Lakini huu ni mchezo ambao haumsubiri mtu na nafikiri hilo linaweza kutokea mwanzoni mwa msimu ujao. sifikiri kama atacheza tena."
Nae nahodha wa zamani wa Barcelona Carles Puyol amekasirika , baada ya real Madrid kushinda Champions League kwa mara ya 13 na kusema klabu hiyo ya Catalonia inapaswa kubadilisha malengo yake msimu ujao. "Naamini tuna kikosi kizuri kuliko Madrid, lakini wameshinda mara nne katika misimu mitano ya Champions League," Puyol aliliambia gazeti la mjini Barcelona la Vanguardia leo Jumatatu.
"Nafikiri suluhisho litakuja baada ya kuweka malengo yetu sawa. Tunapoteza fursa , nimekasirika kuhusu hilo kama shabiki wa Barca. "Kushinda mataji matatu katika msimu ni ngumu mno kama takwimu zinavyoonesha, kwa hiyo nafikiri jambo zuri la kufanya itakuwa kuachana na kombe la Mfalme. Puyol ameongeza kwamba vikombe vingine wapewe nafasi vijana kuonesha uwezo wao na wachezaji wa kikosi cha kwanza washughulike na ligi na Champions League.
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew karibu tayari amekwisha kamilisha kikosi chake cha awali kwa ajili ya mazowezi leo Jumatatu katika kituo cha mazowezi ya timu hiyo cha Eppan nchini Italia.
Mchezaji wa kati ya Real Madrid Tony Kroos antarajiwa kujiunga na kikosi hicho cha mabingwa watetezi wiki hii , wakati mlinzi wa Bayern Jerome Boateng anaendelea kupata nafuu kutokana na maumivu ya paja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman