Real Madrid ndiyo klabu tajiri kabisa duniani
22 Januari 2016Real Madrid imechukua nafasi ya kwanza ikifuatwa na Barcelona kwenye orodha hiyo ya Shirika la Ukaguzi wa Hesabu la Deloitte Football League. Bayern Munich ni timu pekee ya Bundesliga kuwa katika kumi bora.
Mapato ya Madrid yalikua kutoka euro milioni 459.5 hadi 577, wakati Barcelona – ambao wameruka nafasi mbili juu hadi nafasi ya pili – wakiwa na ongezeko kubwa la mapato kutoka euro milioni 484.8 hadi euro milioni 560.8.
Bayern iko katika nafasi za ishirini bora, lakini iliteremka nafasi mbili chini hadi nafasi ya tano, nyuma ya klabu ya Ufaransa Paris Saint-Germain na miamba wa Premier League Manchester United. Mapato ya Bayern yalipungua kwa euro milioni 13 hadi milioni 474 katika msimu wa 2014/15, licha ya kutwaa taji la Bundesliga. Borussia Dortmund na Schalke ni vilabu nyingine mbili za Bundesliga katika ishirini bora, ambapo Dortmund iko katika nafasi ya saba, baada ya mapato yao kuongezeka kwa euro milioni 19.1 hadi euro milioni 280.6. Schalke iko nafasi ya 13 baada ya mapato yao kupanda kwa euro milioni 5.7 hadi euro milioni 219.7
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohamed Khelef