Rasimu ya makubaliano ya Brexit yafafanuliwa
28 Februari 2018Rasimu hiyo ya kurasa 120, inafafanua kwa lugha ya kisheria maridhiano yaliyofikiwa december mwaka jana katika mada tatu muhimu; hatima ya raia wa pande mbili, gharama za talaka na mustakbali wa mpaka wa Ireland.
Rasimu hiyo inafafanua pia kanuni za kipindi cha mpito kilichopendekezwa na Uingereza, baada ya nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa ulaya, mwishoni mwa mwezi Marchi mwaka 2019, ili kuepukana na madhara ya mtengano wa ghafla, huku makubaliano ya kibiashara yakisubiriwa kukamilishwa kati ya pande mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa mawaziri wa Umoja wa ulaya wanaoshughulikia masuala ya Ulaya, mkuu wa tume ya Brexit, Michel Barnier amezungumzia mivutano iliyoko kati ya pande hizi mbili kuhusu mada muhimu. Michel Barnier anasema:"Nnataka kusema na hili nililisema mbele ya mawaziri hapo awali, bado kuna mada kadhaa zinazozusha mabishano pamoja na Uingereza, tukizingatia kile tunachokielewa kuwa ni "kipindi cha mpito", masharti na muda wa kipindi hicho. Kwa sasa muda wa kipindi hicho-tumependekeza umalizike december 31 mwaka 2020, wakati mmoja na kipindi cha bajeti ya miaka mingi. Uingereza inataka kipindi hicho cha mpito kisiwe na mwisho, jambo ambalo haliwezekani".
Kizingiti kikubwa ni pamoja na mpaka kati ya Jamhuri ya Ireland na jimbo la Ireland
Mbali na suala la muda wa kipindi cha mpito, Michel Barnier amezungumzia mada kadhaa pia za mabishano kati ya pande mbili: Suala linalohusu haki ya raia wa nchi za Umoja wa ulaya wanaoishi Uingereza na pia suala la mpaka kati ya jamhuri ya Ireland na jimbo la Uingereza la Ireland ya kaskazini.
Baada ya kutangazwa hadharani hii leo, rasimu hiyo itabidi ijadiliwe na viongozi 27 wa Umoja wa ulaya kabla ya kukabidhiwa viongozi wa mjini London. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza Boris Johnson anasema suala la mpaka kati ya jamhuri ya Ireland na jimbo la Ireland ya kaskazini linatumiwa ili kujaribu kushikilia Uingereza katika umoja wa forodha na kwa namna hiyo kuifanya iwe shida kwa nchi yao kujitoa katika Umoja huo. Akizungumza na kituo cha Sky News, Boris Johnson amesema kuna njia zinazoiruhusu Uingereza kutoka katika umoja wa forodha bila ya kuwa na hatua kali za mpakani katika jimbo la Ireland ya Kaskazini.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel