1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Tunisia afariki dunia

Faiz Musa25 Julai 2019

Rais wa Tunisia Beji Caid Essebsi ameaga dunia katika hospitali ya kijeshi mjini Tunis baada ya kulazwa usiku wa kuamkia leo. Ilikuwa mara ya pili kulazwa hospitali katika kipindi cha mwezi mmoja

https://p.dw.com/p/3MjqD
Obama Meets With Tunisian President Beji Caid Essebsi At White House
Picha: Getty Images

Essebsi amefariki akiwa na umri wa miaka 92. Msemaji wa rais Aida Klibii ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba marehemu Essebsi amefariki mwendo wa saa nne asubuhi hii leo akipokea matibabu. Ukurasa rasmi wa Facebook wa marehemu Essebsi umeandikwa kwamba taarifa za mazishi zitatangazwa muda wowote.

Spika wa bunge la Tunisia, Mohammed Ennaceur ametangaza kushikilia nafasi ya Urais kwa muda.

"Ningependa kuyatilia maanani aliyoyafanya rais Beji Caid Essebsi ya kuijengea nchi hii kuwa huru na vile vile kwa kuwa rais wa taifa hili kwa muda wa miaka mitano. Ningependa kuwakumbusha kwamba serikali itaendelea kulingana na katiba ya Tunisia, mkuu wa bunge atakuwa rais wa mpito," alisema Ennaceur.

Tunesien Präsident Beji Caid Essebsi
Rais wa Tunisia Beji Caid EssebsiPicha: DW/F. Quenum

Kulingana na katiba ya Tunisia, spika wa bunge anachukua nafasi ya urais kwa muda wa siku 45-90 wakati kukiandaliwa uchaguzi mpya, baada ya mahakama ya kikatiba kuthibitisha kwamba nafasi ya rais iko wazi. Kwa sasa nchini Tunisia hakuna mahakama ya kikatiba baada ya bunge kutoelewana juu ya wanachama wake.

Tangu kuingia madarakani mwaka 2014 Essebsi ameonekana mara chache sana na mara ya mwisho kuonekana ilikuwa Jumatatu wiki hii alipokutana na waziri wa ulinzi Abdelkarim Zbidi na alionekana kuwa dhaifu sana kiafya. Kifo chake kimenasibiana na siku ya kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Taifa hilo baada ya kuuondoa utawala wa kifalme, sherehe za kuadhimisha siku hiyo leo zimefutiliwa mbali.

Jumuiya ya kimataifa yamsifu Essebsi

Waziri mkuu wa Tunisia Youssef Chahed ametangaza siku saba za maombolezi ambapo bendera zitapepeprushwa nusu mlingoti. Radio na Runinga nchini humo zimesimamisha vipindi vyake na kuchezesha kisomo cha Quran.

Tume ya uchaguzi ya Tunisia imetangaza kwamba kutokana na kifo hicho uchaguzi wa uraisi utafanyika mapema kinyume na ulivyotarajiwa Novemba 17.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemtaja Essebsi kuwa shujaa katika njia ya kuweka demokrasia huku waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte akituma salamu zake za rambirambi katika mtandao wake wa kijamii wa Twita akimtaja marehemu kama mwanchi aliye na ubindamu mkubwa.

Marehemu Essebsi, ni kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia Tunisia mwaka 2014 baada vuguvugu la mabadiliko katika mataifa ya kiarabu. Aliingia katika siasa mwaka 1940 na alikuwa wakili, alisomea taalum hiyo Paris - Ufaransa. Anahusishwa sana na rais wa kwanza wa Tunisia, Habib Bourguiba aliyejenga nchi hiyo na kuwaelimisha watu wake.

(DPAE/RTREAPE)