Rangoon. Baraza la haki za binadamu lashutumu matumizi ya nguvu Burma.
3 Oktoba 2007Baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa limepitisha azimio linaloshutumu matumizi ya nguvu wiki iliyopita dhidi ya waandamanaji wanaodai demokrasia yaliyofanywa na jeshi la Burma. Baraza la haki za bindamu la umoja wa mataifa pia limeutaka utawala wa kijeshi wa Burma kumruhusu mchunguzi wake kuzuru nchini humo kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka minne. Paulo Sergio Pinheiro, mwakilishi maalum wa umoja wa mataifa kwa ajili ya hali ya haki za binadamu nchini Burma , amekiambia kikao hicho maalum cha baraza hilo mjini Geneva kuwa yuko tayari kuchunguza na kuripoti kwa baraza hilo lenye wajumbe 47.
Wakati huo huo mwakilishi maalum wa umoja wa mataifa Ibrahim Gambari ameondoka nchini Burma baada ya kukutana na viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo pamoja na kiongozi maarufu wa upinzani Aung San Suu Kyi. Hakuna maelezo yaliyotolewa hadi sasa kuhusiana na mkutano wa Gambari na jenerali Than Shwe , lakini mjumbe huyo wa umoja wa mataifa alipeleka ujumbe wa jumuiya ya kimataifa dhidi ya matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.