Ramallah,Bwana Qurei Baraza lake jipya la Mawaziri laungwa mkono na Fatah.
24 Februari 2005Hatimaye Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina,Ahmed Qurei amepata idhini kutoka kikundi kikubwa cha Wapalestina cha Fatah kwa ajili ya majina aliyoyapendekeza yatakayounda Baraza lake jipya la Mawaziri.Kwa muda wa siku tatu mfululizo mawaziri kutoka kikundi cha Fatah walikuwa wamegoma kuliidhinisha Baraza hilo jipya hadi Bwana Qurei alipotakiwa kuwajumuisha wapenda mageuzi wengi ndani ya Baraza hilo na kuwapa nafasi chache wanasiasa wakongwe waliokuwa tangu enzi za marehemu Yasser Arafat ambao machoni pa Wapalestina wengi wanaonekana ni watu wanaokumbatia sana vitendo vya rushwa.
Bwana Qurei alikuwa anakabiliwa na hatari ya kupoteza wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu baada ya Wabunge wa upande wa kikundi cha Fatah kuyakataa majina aliyoyapendekeza ambapo kulikuwa na sura mpya nne tu.
Maofisa wa Palestina wamesema kwa sasa karibu robo tatu ya waliomo katika Baraza jipya la Mawaziri ni wapya kabisa na ambao ni wataalam waliobobea wanaonekana kuwa watamudu kumaliza kero za rushwa na nyingine za kijamii.Baraza hilo jipya la Mawaziri linatazamiwa kuidhinishwa leo.