Ramallah: Waziri wa mambo ya nje wa Marekani awasili ukingo wa magharibi wa Mto Jordan.
2 Agosti 2007
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Condoleezza Rice amewasili mjini Ramallah katika Ukingo wa magharibi wa mto Jordan.
Bi Codoleezza Rice amekutana na kaimu Waziri Mkuu wa Palestina, Salam Fayyad, kwenye harakati zake za kujaribu kuandaa mkutano unaolengwa kufufua mashauriano yaliyokwama ya amani kati ya Wapalestina na Israil.
Bi Condoleezza Rice amesema:
"Yaliyotendeka Gaza yalikuwa kinyume cha matakwa ya umma wa Palestina. Kamwe hatutawaacha mkono wakazi wa Gaza. Tutaendelea kuwapelekea msaada wananchi wa Gaza kwa misingi ya kibinadamu. Tunajua kuna watu wengi wasio na hatia wanaoishi katika eneo hilo"
Bi Condoleezza Rice amepangiwa pia kukutana na Rais Mahmoud Abbas.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani aliwasili nchini Israil jana kutokea nchini Saudi Arabia na akasema ameridhishwa na jinsi viongozi wa kiarabu na Israil walivyoyazingatia mapendekezo ya Rais George Bush ya kuandaa kikao cha kanda hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu.