Rajoelina kurejesha demokrasia halisi Madagascar
18 Machi 2009Jumuiya ya kimataifa imeshtushwa na jinsi Rajoelina alivyopuuza uamuzi wa wananchi wengi na kumtimua madarakani Marc Ravalomanana aliechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.Rajoelina aliemshutumu Ravalomanana kuwa amekandamiza demokrasia kwa kuzuia uhuru wa vyombo vya habari na kutumia nguvu zilizopindukia kiasi dhidi ya raia, binafsi ametegemea jeshi na raia mitaani kumweka madarakani badala ya kuitisha uchaguzi. Tangu aliposhinda kwa wingi mkubwa uchaguzi wa meya wa mji mkuu, Antananarivo, Desemba mwaka 2007, Rajoelina ameitumia hali ya kutoridhika miongoni mwa wananchi waliovunjwa moyo na Ravalomanana.
Milionea Ravalomanana alietajirika kwa biashara yake binafsi ya mazao ya maziwa alishangiliwa aliposhika madaraka katika mwaka 2002 kufuatia maandamano yaliyofanywa mitaani. Lakini tofauti ni kuwa yeye alimshinda dikteta Didier Ratsiraka katika uchaguzi uliofanywa mwaka mmoja kabla. Ravalomanana amesifiwa na nchi za Magharibi kwa hatua alizochukua kuruhusu uwekezaji wa kigeni na kusimamia ukuaji wa kiuchumi. Lakini wananchi walihisi kuwa kiongozi wao hakuchukua hatua za kutosha kukabiliana na tatizo la umasikini wakati umma ukishindwa kujipatia riziki ya kutia tumboni kwa sababu ya kuongezeka kwa bei za vyakula.
Madaraka ya Ravalomanana yalianza kuyumbayumba alipojaribu kumzima Rajoelina Desemba iliyopita kwa sababu ya kutangaza mahojiano yaliyofanywa na Ratsiraka aliye uhamishoni. Maandamano ya kupinga kufungwa kwa stesheni ya televisheni ya Rajoelina yakatumiwa na mwanasiasa huyo kijana kuwa kampeni ya kumtimua madarakani Ravalomanana.Akajitangaza rais na akaiteua serikali yake ya mpito huku akiwatumia waandamanaji barabarani kwa kuwapa vyeo huku akiepusha matumizi ya nguvu.Leo ndio Mahakama ya Katiba ya Madagascar imemuidhinisha Rajoelina kuchukua nafasi ya Ravalomanana. Baadae,Rajoelina alipohutubia umati wa kama watu 10,000 katika mji mkuu Antananarivo aliahidi kurejesha demokrasia halisi.Amesema:
"Tuko tayari kubeba dhamana zetu, jukumu letu la kuiongoza nchi yetu. Hivi sasa tutafanya kila liwezekanalo kuunda utawala wa mpito na serikali ya mpito itakayotawala na itakayotayarisha uchaguzi wa urais unaotazamiwa kufanywa katika muda usiopindukia miezi 24."
Akaongezea kuwa rais wa zamani atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhalifu na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji katika majuma ya hivi karibuni. Lakini lengo lake kuu amesema ni kupata umoja wa kitaifa na kuyafungamanisha makundi mbali mbali ya kiasili nchini humo. Wadadisi wanasema kwamba hatua ya kumuidhinisha Rajoelina huenda ikasaidia kurejesha utulivu nchini humo lakini hali hiyo,haitodumu ikiwa wananchi watavunjwa moyo na Rajoelina vile vile.
Mwandishi: P.Martin
Mhariri: O.Miraji