1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rajoelina achukua hatamu za uongozi wa mpito Madagascar

Thelma Mwadzaya18 Machi 2009

Uongozi wa kijeshi nchini Madagascar umemuidhinisha rasmi kiongozi wa upinzani Andry Rajoelina kuwa rais wa kipindi cha mpito saa chache baada ya rais Ravalomanana kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/HEhO
Kiongozi wa upinzani Andry RajoelinaPicha: AP


Hapo jana Ravalomanana alimkabidhi madaraka ya uongozi naibu mkuu wa jeshi la wanamaji Hyppolite Ramaroson lakini mkuu huyo wa jeshi ametangaza kwamba jeshi limekataa kutawala na badala yake kumpa jukumu hilo Rajoelina.


Uongozi wa juu wa kijeshi ulioachiwa madaraka na rais Ravalomanana baada ya kutangaza kujiuzulu hapo jana umeyakabidhi madaraka hayo kwa kiongozi wa upinzani Andry Rajoelina .Naibu mkuu wa majeshi ya wanamaji Hippolyte Ramaroson amewaambia waandishi wa habari kwamba kundi la uongozi wa kijeshi nchini humo unatoa hatamu za uongozi kwa Rajoelina kuwa rais wa kipindi cha mpito.


Kabla ya hapo upinzani ulisema kwamba jeshi limemkamata naibu huyo mkuu wa jeshi la wanamaji pamoja na viongozi wengine wa kijeshi kwa shutuma za kuwa vibaraka wa rais Ravalomanana.Rais Ravalomanana hadi sasa hajulikani aliko baada ya kujiuzulu huku ubalozi wa Marekani mjini Antananarivo ukikanusha kwamba umempa hifadhi kiongozi huyo.

Nchi za kiafrika katika kanda hiyo zimeyakosoa mabadiliko hayo ya uongozi zikisema kwamba ni hatua isiyo ya kidemokrasia.Rais wa Afrika kusini Kgalema Motlante anayeongoza jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC amesisitiza kwamba jumuiya hiyo hatokubali vitendo vya kukiuka demokrasia.Umoja wa ulaya umeshaonya kwamba huenda wakaisusia nchi hiyo ikiwa Ravalomanana ataondolewa madarakani huku Marekani ikitishia kusitisha msaada wake kwa nchi hiyo.


Taarifa kutoka nchini Madagascar zinasema kiongozi huyo wa upinzani Andry Rajoelina ameshamthibitisha Monja Roindefo kuwa waziri mkuu wa kisiwa hicho cha bara hindi.Roindefo ameyataja mabadiliko hayo ya uongozi nchini humo kuwa ni hatua ya kuanza enzi mpya.

''Nchini Madagascar mtoto amezaliwa,mabadiliko mapya yameingia na kile tunachokifanya hivi sasa ni kurudisha demokrasia hapa Madagascar.''


Kutokana na hatua ya jeshi ya kukataa kuchukua hatamu za uongozi nchini humo kama alivyotaka Ravalomanana inaamaanisha kwamba sasa Umoja wa Afrika huenda ukashindwa kutangaza hatua ya Rajoelina kuwa ni mapinduzi lakini kwa upande mwingine kuangushwa huko kwa Ravalomanana kumeongeza shakashaka juu ya uthabiti wa demokrasia katika nchi nyingine za kiafrika.


Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo kiongozi wa bunge angepaswa kuchukua madaraka na kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi miwili.Hali ya mambo katika mji mkuu Antananarivo inasemekana kuwa shwari Jeshi limesema litaendelea na juhudi zake za kuweka amani nchini humo.Kanali Andre Dria Regione ni msemaji wa jeshi la Madagascar.''Jeshi litajitahidi wakati huu muhimu kabisa kurejesha hali ya utulivu na amani katika kisiwa hiki.''


Baadhi ya wadadisi wanasema kuondoka kwa Ravalomanana huenda bila shaka kukamaliza ghasia angalau kwa sasa nchini humo na kuleta mazingira yatakayowavutia wawekezaji wa kigeni katika sekta muhimu za madini na mafuta.


Ravalomanana aliingia tena madarakani kuongoza muhula wa pili mwaka 2006 na chini ya utawala wake alifanikiwa kuwavutia wawekezaji wa kigeni na hasa katika sekta ya madini lakini idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo wanaishi katika hali ya umaskini mkubwa jambo ambalo alilitumia mpinzani wake Rajoelina kuwashawishi wafuasi wengi.Rajoelina mwenye umri wa miaka 34 anasema Ravalomanana alikuwa anatumia vibaya fedha za umma.

AFPE