Raisi aonya waandamanaji nchini Iran
23 Septemba 2022Msichana huyo wa miaka 22 alikuwa akizuiwa kwenye kituo cha polisi wa maadili nchini humo.
Alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, rais Ebrahim Raisi amesema tayari ameagiza kufanyika uchunguzi wa tukio hilo la Mahsa aliyefariki wiki moja baada ya kukamatwa kwa madai ya kuvaa mavazi yasiyokubalika.
Alinukuliwa akisema kuna uhuru wa kujieleza Iran, lakini vitendo vya vurugu havikubaliki.
"Bila shaka, haya ni ya kawaida na yaliyotarajiwa kabisa, lakini ni lazima tutofautishe kati ya waandamanaji na waharibifu. Maandamano ni mazuri kwa sababu watu fulani wanaweza kuwa na maoni ambayo wangependa kuyatoa kuhusu masuala mahususi. Kuna mambo leo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mambo ambayo yanajadiliwa, mambo ambayo ndani yake kuna maoni mengi tofauti." alisema Raisi.
Aidha kiongozi huyo amesisitiza kwamba Amini hakuteswa na polisi, ingawa amesema, bado analifuatilia na iwapo kulikuwepo na mapungufu ni lazima kutafanyika uchunguzi.
Kwa upande mwingine, Raisi ameyatuhumu mataifa ya magharibi kwa undumila kuwili na kuchochea hali ya wasiwasi na hasa baada ya kuiwekea vikwazo idara hiyo ya kipolisi, huku akinyooshea kidole mauaji yanayofanywa na polisi nchini Marekani na vifo vya wanawake nchini Uingereza.
Kikosi cha Walinzi wa Kimapinduzi chenye ushawishi mkubwa nchini Iran kimeitolea mwito mahakama kuwashitaki wote wanaosambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii na mitaani, likisema wanahatarisha usalama wa kisaikolojia wa jamii, na kuitaka mahakama kuwakabili ipasavyo.
Mkuu wa mahakama Gholamhossein Mohsein Ejei ameagiza kuendeshwa haraka kwa kesi za waandamanaji ili kuimarisha usalama na amani kwa raia.
Wizara ya intelijensia ya Iran pia imejaribu kuyazuia maandamano hayo ikionya ni kinyume cha sheria kushiriki kwenye maandamano na yoyote anayeandamana atafunguliwa mashitaka, hii ikiwa ni kulingana na tovuti za habari za Iran.
Haya ni maandamano makubwa kabisa kushuhudiwa kwenye taifa hilo la Kiislamu tangu mwaka 2019, huku wanawake waliojitokeza kwa kiasi kikubwa wakichoma moto hijabu zao.
Sikiliza Zaidi:
Kifo cha Amini kimechochea ghadhabu dhidi ya masuala ambayo ni pamoja na vizuizi katia uhuru binafsi nchini Iran ikiwa ni pamoja na mavazi kwa wanawake na uchumi uliozoroteshwa na vikwazo. Viongozi wa dini wanahofia kurejea kwa maandamano makubwa kabisa kama ya mwaka 2019 yaliyoibuka baada ya kuongezeka kwa gharama za gesi ambapo mamia ya waandamanaji waliuawa.
Mashirika: RTRE/AFPE