Rais wa zamani wa Kenya, Daniel Arap Moi ameaga dunia
4 Februari 2020
''Taifa letu na bara letu, vilipata bahati ya kuwa na Moi, mtu aliyejitolea maisha yake yote ya utu uzima kuitumikia Kenya na Afrika.'' Amesema Rais Kenyatta katika tangazo lake kwa taifa.
Mtoto mkubwa wa Moi, Gideon Moi ambaye ni seneta, amesema baba yake amekufa kwa amani akiwa amezungukwa na familia yake hospitalini, saa kumi na moja na dakika ishirini (11.20) alfajiri. Gideon Moi pia ametoa shukrani za familia yake, kwa Wakenya wote waliomuombea marehemu baba yake.
Hakubainisha kilichosababisha kifo chake, lakini kwa azidi ya mwezi mmoja amekuwa amelazwa hospitalini akipatiwa matibabu.
Rais Kenya amesema ameamuru bendera zote nchini Kenya kupepea nusu mlingoni kuomboleza kifo cha kiongozi huyo. ''Moi alitekeleza vizuri majukumu yake, alikuwa mtu wa imani, na hivi sasa anafurahia tuzo yake mbinguni.'', amesema Kenyatta, na kuongeza kuwa atapewa mazishi yenye heshima zote za kijeshi na kiraia.
Moi aliongoza Kenya kuanzia mwaka 1978 hadi 2002, utawala wake chini ya mfumo wa chama kimoja ukigubikwa na madai ya mienendo ya kiimla, uvunjifu wa haki za binadamu na ubadhirifu.
Licha ya shutuma hizo lakini, aliungwa mkono na Wakenya wengi kama nguzo ya umoja na utangamano katika taifa lake.
Wanadiplomasia wanasema jaribio la mapinduzi dhidi yake miaka minne baada ya kuingia madarakani, lilishawishi siasa zake za kutawala kwa mkono wa chuma.
Kabla ya kuwa rais, Daniel Arap Moi alikuwa makamu wa rais wa Kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta.
rtre, ape