Rais wa Urusi Vladimir Putin aitembelea Crimea
9 Mei 2014Rais Putin amewasili katika uwanja wa ndege wa Belbek karibu na Sevastopol kituo cha jadi cha manuari za Urusi katika bahari nyeusi.Hii ni ziara yake ya kwanza katika raasi ya Crimea-eneo la Ukraine lililomezwa na Moscow mwezi machi mwaka huu. Rais Putin amekagua gwaride la kijeshi huko Sebastopol katika sherehe za kuadhimisha "siku ya ushindi dhidi ya utawala wa wanazi",mwaka 1945 kabla ya kuwahutubia umati wa watu waliokusanyika .
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliukosoa hapo awali mpango wa rais Putin wa kuitembelea Crimea katika wakati ambapo eneo la mashariki na lile la kusini la Ukraine linazidi kuzama katika bahari ya machafuko.Ikulu ya Marekani pia imeikosoa ziara hiyo na kusema "inazidisha mashaka".
NATO inaendelea kuiangalia Crimea kuwa ni milki ya Ukraine
Lawama kama hizo zimetolewa pia na katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen aliyeitaja ziara ya Putin huko Crimea kuwa "isiyofaa" na kuongeza "jumuia ya NATO ingali inaitambua raasi ya Crimea kuwa ni milki ya Ukraine."
Serikali ya mjini Kiev na nchi za magharibi zinaituhumu Moscow kupalilia kujitenga kwa maeneo hayo.Serikali ya mjini Kiev imelalamika vikali dhidi ya ziara ya rais Putin katika eneo hilo lililojitenga la Crimea .
Mapigano yamepamba moto mashariki ya Ukraine
Mapigano yameripotiwa katika mji wa bandari wa kusini mashariki-Marioupol kati ya vikosi tiifu kwa serikali ya Ukraine na wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi na kuangamiza maisha ya watu kadhaa.Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ukraine watu wasiopungua 20 wakiwemo wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wameuwawa.Vikosi vya serikali vilikuwa vinataka kuyakomboa makao makuu ya polisi ya mji huo wa bandari yaliyokuwa yakidhibitiwa na waasi.Makao makuu hayo yametiwa moto.
Mapigano yameripotiwa pia katika miji ya Luhansk na Kramatorsk katika wakati ambapo vikosi vya serikali vinaendelea kuuzingira mji wa Sloviansk unaodhibitiwa na waasi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/AP
Mhariri:Yusuf Saumu