1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Umoja wa Ulaya atoa raia kwa bunge la Ulaya baada ya kura ya Ireland.

18 Juni 2008

Asema mkutano wa kilele wa umoja wa Ulaya mwishoni mwa juma hili hauna budi kushinikiza juu ya matatizo ya wakati huu.

https://p.dw.com/p/EMLB
rais wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.Picha: AP

Bw Barroso alikua akilihutubia bunge la Ulaya mjini Strasbourg leo na akautaka mkutano ujao wa viongozi wakuu wa umoja wa Ulaya, uzingatia masuala kama kupanda bei ya mafuta na kuonyesha kwamba ´kukataliwa makubaliano ya Lisbon katika kura ya maoni huko Ireland hivi karibuni sio mwisho wa Ulaya.

Akaonya kwamba kura ya hapana kuhusiana na mkataba wa Lisbon katika Jamhuri ya Ireland isiwe sababu ya kuporomoka kwa ulaya. Alisema "katika wakati huu ambapo bei ya chakula na mafuta zinaongezeka mno, hatuwezi kuweka kando tatizo hilo."

Rais huyo wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya,akasema njia bora ya kukamilisha mradi huo ni kuzishughulikia nyanja muhimu, ambapo umoja wa ulaya unaweza kupata mafanikio.

Akizungumza katika kikao cha bunge hilo la ulaya, huku baadhi ya wakati akikatizwa kwa makelele ya wabunge na wengine wakiinua fulani za kijani zilizokua na maandishi " Heshimu kura ya Ireland." Barosso aliongeza kwamba inabidi umoja wa ulaya uchukue mtazamo madhubuti kwa kuzingatia nyenzo ulizonazo, kuweza kuzaa matunda katika kipindi kifupi, cha wastani na katika kipindi kirefu.

Bw Barroso akataja mlolongo wa hatua za dharura zinazoweza kuwasaidia watu wa ulaya kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, akisisitiza tena kura ya hapana nchini Ireland ambayo mezusha pigo kubwa kwa mkataba wa Lisbon unaolenga katika kuurekebisha umoja huo uliotanuliwa, isiwe sababu ya kutochukua hatua.

Mnamo wiki iliopita asili mia 53.4 ya wapiga kura wa Ireland waliupinga mkataba huo wa Marekebisho, kwa madhumuni ya kuchukua nafasi ya katiba ya umoja wa Ulaya ilioangushwa baada ya kukataliwa na wapiga kura nchini Ufaransa na Uholanzi 2005.

Wengi wa wabunge wa bunge la Ulaya waliojibu hotuba ya Bw Barroso waliunga mkono wito wa umoja huo wa kusaka suluhisho la masuala yanayoukabili wakati huu. Hata hivyo kiongozi wa wabunge wa Kisoshalisti Martin Shultz kutoka Ujerumani ,alimtaka kamishna wa umoja huo Charlie McCreevy aondolewe katika wadhifa wake akimshutumu kuwa alichangia katika kukataliwa kwa makubaliano ya Lisbon na wapiga kura nchini mnwake, baada ya Bw McCreevy kusema hata hajausoma mkataba huo wa Lisbon.

Hata hivyo Bw Barroso alijibu akisema na hapa ninamnukuu "matamshi ya Bw McCreevy si jambo lililotarajiwa, lakini kumshambulia kamishna huyo anayehusika na biashara ya ndani sio njia bora ya kuzungumza na marafiki zetu wa Ireland."

Mkataba wa Lisbon uliopangwa kuanza kazi mapema mwaka ujao, ulipaswa kwanza kukubaliwa na nchi zote 27 wanachama wa umoja wa Ulaya.Hadi sasa nchi 18 zimeshauidhinisha kupitia bungeni yao ya kitaifa.