Rais wa Ujerumani ziarani barani Asia
1 Februari 2010Matangazo
Nchini India Köhler atajaribu kuishirikisha India katika jitahada za kurekebisha masoko ya fedha duniani na kushughulikia mwongozo mpya wa kimataifa. Hiyo pia itakuwa mada kuu wakati wa ziara yake ya Korea ya Kusini.
Ziara hiyo ya siku kumi barani Asia, inampeleka Rais wa Ujerumani Horst Köhler katika nchi mbili zilizo tofauti kabisa. Korea ya Kusini ambayo miaka 50 ya nyuma ilikuwa masikini na sasa inajitamba kuwa miongoni mwa nchi tajiri zilizostawi kiuchumi duniani. Kwa upande mwingine, India ingali ikipambana na umasikini mkubwa na mivutano ya kijamii. Asilimia 80 ya wakazi wa India wanaishi kwa kutumia chini ya dola 2.50 kwa siku.
Lakini India iliyoshuhudia ukuaji wa kiuchumi wa asilimia 8 mwaka uliopita, ni nchi inayoivutia Ujerumani kibiashara anasema mtaalamu wa masuala ya India katika Taasisi ya Sayansi na Siasa Christian Wagner na kuongezea:
" Baada ya India kufungua masoko yake, wafanya biashara wengi wa Kijerumani pia wamegundua fursa ya kuingia katika masoko ya India. Vile vile kuna sekta ya teknolojia na sayansi. "
Mtaalamu huyo anaeleza kuwa kila mwaka vyuo vyikuu nchini India vinatoa wahandisi kwa maelfu na makampuni ya Kijerumani yanazidi kuhamisha huduma zake nchini India. Siku hizi hata vyuo vya ufundi vya Ujerumani vinazidi kushirikiana na taasisi za elimu na utafiti nchini India.
Hata Rais Köhler aliefuatana na tume ya wafanyabiashara wa ngazi za juu atakutana na wajumbe wa vyuo vya sayansi na ufundi wakati wa ziara yake katika mji mkuu New Delhi na mji wa biashara Mumbai.
Siku ya Jumapili, Köhler ataelekea mji mkuu wa Korea ya Kusini Seoul. Mwaka huu, nchi hiyo ni mwenyekiti wa kundi la nchi 20 tajiri zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi duniani G-20. Mkutano wa kilele wa kundi hilo la G-20 umepangwa kufanywa Seoul wakati wa majira ya mapukutiko. Wataalamu wanasema uchumi wa Korea ya Kusini upo njiani kuimarika baada ya kuporomoka wakati wa msukosuko wa fedha na uchumi duniani. Serikali ya nchi hiyo katika mipango yake ya kuimarisha uchumi hasa imetilia mkazo miradi inayohusika na uchumi endelevu na unaozingatia mazingira. Rais Köhler wakati wa ziara yake hiyo atakutana pia na wajumbe wa sekta ya biashara mjini Seoul.
Mwandishi:Marx,Bettina/ZPR/P.Martin
Mhariri: M. Abdul-Rahman
Matangazo