Gauck kukutana na Obama
7 Oktoba 2015Bwana Gauck amesema ikiwa watu ni wakweli watakubali kwamba uhusiano baina ya Marekani na Ulaya haukushughulikiwa kwa uangalifu wa kiasi kilichokuwa cha lazima.
Akihutubia kwenye chuo kikuu cha Pennysylvania mjini Philadelphia Gauck alisisitiza kuwa mfungamano na Marekani ndiyo nguzo ya uwepo wa Ulaya huru, ikiwa pamoja na Ujerumani.
Kiongozi huyo wa Ujerumani ametilia maanani kwamba mfungamano wa kijeshi wa NATO sasa unakabiliwa na changamoto mpya,kama vile ugaidi ,kuibuka kwa madikteta,kuanguka kwa mataifa na sehemu zinazotumbukia katika vurumai.
Rais wa Ujerumani anaetarajia kukutana na Rais Obama baadae leo pia ameitaka Marekani ijihusishe zaidi na mgogoro wa wakimbizi unaolikabili bara la Ulaya. Amesema mjadala juu ya mgogoro wa wakimbizi haupaswi kuwa suala la Ulaya peke yake, na ametamka wazi kwamba kujiingiza kwa Marekani katika Mashariki ya Kati kumechangia kuleta vurumai iliyowafanya maalfu ya watu waikimbie sehemu hiyo.
Hii ni mara ya kwanza,baada ya miaka 18,kupita kwa Rais wa Ujerumani kukutana na Rais wa Marekani kwenye Ikulu ya nchi hiyo. Rais Gauck pia atakutana na Makamu wa Rais, Joe Biden na Waziri wa mambo ya nje John Kerry.
Marekani iyafuate maadili inayoyahubiri
Rais wa Ujerumani aliuchagua mji wa Philadelphia kuwa kituo cha kwanza cha ziara yake ya Marekani kutokana na umaarufu wa mji huo kuwa chimbuko la demokrasia nchini Marekani. Ni katika mji huo ambako waanzilishi wa taifa la Marekani waliliandika tamko la uhuru.
Katika hotuba yake Bwana Gauck pia aliitaka Marekani irejeshe imani iliyoipoteza kutokana na kashfa ya udukuzi wa simu za wananchi wa Ujerumani uliofanywa na idara ya Marekani ya usalama wa taifa. Ameitaka Marekani iyafuate maadili ambayo yenyewe inayahubiri.
Mwandishi:Mtullya abdu/ZA,DPA,
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman