1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ufaransa haondoi uwezekano wa kususia ufunguzi wa michezo ya Olimpiki.

27 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DVpQ

London.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown wametoa wito leo kwa mabenki kuweka wazi kiasi cha uharibifu uliotokea katika shughuli zao zilizosababishwa na kuporomoka kwa uwezo wa ukopeshaji.

Viongozi duniani kote wanajaribu kuzuwia mtafaruku wa kuporomoka zaidi, katika hali ya wasi wasi wa taasisi za fedha za kimataifa uliotokana na madeni ambayo hayajalipwa na nyumba nchini Marekani na kuleta kitisho cha kuharibika kwa uchumi wa dunia.

Brown na Sarkozy wamesema katika mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kuwapo haja ya kuwa wazi zaidi masoko ya fedha ili kuhakikisha kuwa benki zinaweka wazi kila kitu katika kiwango cha madeni yaliyofutwa, ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za kutoa uhakika zaidi wa thamani ya mali ya kifedha.

Wakati huo huo viongozi hao wawili wametofautiana katika suala la wito wa kususiwa ufunguzi wa michezo ya Olimpiki nchini China.

Wakati Bwana Sarkozy amesema kuwa yeye haondoi uwezekano wa kususia ufunguzi wa michezo ya Olimpiki, ambayo itafanyika wakati akiwa rais wa umoja wa Ulaya , Bwana Brown amesema Uingereza haitasusia ufunguzi wa michezo hiyo mjini Beijing.

Sarkozy amesema kwa kuwa Ufaransa itakuwa rais wa umoja wa Ulaya wakati huo atawashauri wanachama wengine wa umoja huo kuona iwapo kuna haja ama la ya kususia.