Ufaransa kuwaondoa wanajeshi wake walioko Niger
25 Septemba 2023Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza jana Jumapili kwamba Ufaransa itawaondoa wanajeshi wake nchini Niger pamoja na kumrejesha nyumbani balozi wake baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais Mohamed Bazoum.
Tangazo hilo, ni pigo kubwa dhidi ya sera za Ufaransa barani Afrika, baada ya wanajeshi wa taifa hilo pia kuondoka taifa jirani la Mali na Burkina Faso katika miaka ya karibuni baada ya kukumbwa na mapinduzi.
Ufaransa iliwabakiza wanajeshi wake 1,500 nchini Niger tangu mapinduzi ya Julai na mara kadhaa imekaidi agizo la utawala mpya wa kijeshi la kumuondoa balozi wake, kwa kuwa Ufaransa haiutambui utawala huo.
Soma pia: Raia waandamana Niger kutaka Ufaransa iondoe wanajeshi wake
Taifa hilo lilipeleka maelfu ya wanajeshi kwenye ukanda wa Sahel baada ya wakuu wa mataifa hayo kuiomba kusaidia harakati zao za kupambana na ugaidi.
Utawala wa kijeshi wa Niger wafurahishwa na tangazo la kuondolewa wanajeshi wa Ufaransa
Watawala wa kijeshi wa Niger jana Jumapili walikaribisha tangazo hilo la Ufaransa ikilitaja kama "hatua mpya kuelekea uhuru".
Utawala huo ulitoa kauli hiyo saa chache baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutangaza pia kwamba hivi karibuni Paris itamuondoa balozi wake kutoka Niger, katika miezi ijayo.
"Jumapili hii, tunasherehekea hatua mpya kuelekea uhuru wa Niger," ilisema taarifa ya watawala wa kijeshi wa nchi hiyo, walionyakua mamlaka mwishoni mwa Julai kwa kumpindua rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26.
"Wanajeshi wa Ufaransa na balozi wa Ufaransa wataondoka katika ardhi ya Niger ifikapo mwisho wa mwaka," imeongeza taarifa hiyo iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa: "Huu ni wakati wa kihistoria, ambao unazungumzia dhamira na mapenzi ya watu wa Niger."
Soma Pia: Mkuu wa Jumuiya ya ECOWAS apendekeza kipindi cha miezi 9 nchini Niger
Mapema Jumapili, kabla ya tangazo la Macron, chombo kinachosimamia usalama wa anga barani Afrika (ASECNA), kilitangaza kuwa watawala wa kijeshi wa Niger wamepiga marufuku "ndege za Ufaransa" kuruka juu ya anga ya nchi hiyo.
Mvutano umeongezeka katika wiki za hivi karibuni kati ya Ufaransa na Niger, ambayo nikoloni la zamani la Ufaransa.
Ali Sekou Ramadan, msaidizi wa Rais aliyeondolewa madarakani wa Niger Mohamed Bazoum, aliiambia shirika la habari la Associated Press kwamba Bazoum alimuomba Macron kumwondoa balozi wa Ufaransa, Sylvain Itte, "ili kupunguza mvutano."