Rais wa Somalia Mohamed Farmajo akubali kuitembelea Kenya
10 Machi 2020Farmaajo, aliyeupokea ujumbe maalum kutoka kwa rais Kenyatta mjini Mogadishu hakutangaza siku ambayo atazuru Kenya.
Taarifa kutoka kwenye makazi rasmi ya rais huyo mjini Mogadishu, ilisema kuwa Farmajo, amekubali wito wa rais Kenyatta wa kuwa na mkutano jijini Nairobi.
Hata hivyo taarifa hiyo ya Somali haikutaja suala la mtoro wa jimbo la Jubbaland Abdirashid Hassan Abdinur Janaan aliyekuwa waziri wa usalama.
Janaan alitoroka jela ya Mogadishu na ndiye chanzo cha Mogadishu kupeleka wanajeshi eneo la Gedo karibu na jimbo la Mandera lililoko Kenya.
Waziri wa Usalama wa Taifa, Fred Matiang'i na ujumbe wa maafisa wa usalama walitumwa Jumapili asubuhi kutafuta ufumbuzi wa mzozo kati ya jeshi la Somalia na lile la jimbo la Jubbaland uliovuka mipaka na kuingia nchini Kenya.