1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Somalia amuachisha kazi Waziri Mkuu

Saleh Mwanamilongo
27 Desemba 2021

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohammed almaarufu Farmajo, ametangaza kumuachisha kazi waziri mkuu Mohamed Hussein Roble siku moja baada mabishano baina yao.

https://p.dw.com/p/44rXv
Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed | Farmajo
Picha: Str/AFP

Taarifa kutoka kwa ofisi ya rais imesema kuwa rais Farmajo aliamua kumuachisha kazi Roble na kusitisha madaraka yake kwa sababu ya kuhusishwa kwake na ufisadi na pia kumshtumu kwa kuingilia uchunguzi kuhusu kesi ya unyakuzi wa ardhi.

Roble, ambaye bado hajajibu tangazo hilo la kumuachisha kazi amesema kuwa Farmajo hataki kuandaa uchaguzi wa kuaminika nchini humo.

Kwa upande wake,Rais Farmajo amemshtumu Roble kwa kujaribu kushawishi uchunguzi wa kashfa iliyohusisha ardhi inayomilikiwa na jeshi baada ya waziri huyo mkuu kumfukuza kazi waziri wa ulinzi hapo jana na kumteua mrithi wake.

Soma pia:Viongozi kuharakisha mchakato wa uchaguzi Somalia 

Mivutano isiokwisha baina ya rais na waziri mkuu

Uhusiano kati ya rais Farmajo, na waziri mkuu Roble umekuwa wa mivutano kwa muda mrefu, huku matukio ya hivi punde yakiibua hofu mpya juu ya utulivu wa Somalia wakati inajitahidi kuandaa uchaguzi.

Taarifa ya Ikulu ya rais ya leo Jumatatu inasema waziri mkuu amemshinikiza waziri wa ulinzi kugeuza uchunguzi wa kesi inayohusiana na ardhi ya umma iliyonyakuliwa.

Msaidizi wa Waziri wa Habari Abdirahman Yusuf Omar Adala amesema kupelekwa kwa vikosi vya usalama karibu na ofisi ya  waziri mkuu haitomzuia Roble kutekeleza majukumu yake.

Adala amesema kwenye kurasa wake wa facebook kwamba kinachoendelea asubuhi ya leo ni mapinduzi yasiyo ya moja kwa moja ambayo amesisitiza kuwa hayatafanikiwa.

Wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa 

Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble asema rais hataki uchaguzi wa kuaminika
Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble asema rais hataki uchaguzi wa kuaminikaPicha: Feisal Omar/REUTERS

Marekani imetoa wito wa kuwepo stahamala. Kwenye mtandao wake wa twitter ubalozi wa Marekani nchini Somalia umesema Marekani imewaomba sana viongozi wa Somalia kuchukua hatua za haraka ili kupunguza mvutano huko Mogadishu, kujiepusha na vitendo vya uchochezi, na kuepuka vurugu.

Kwa miezi kadhaa uchaguzi huo wa nchini Somalia umeahirishwa. Mwezi Aprili, wapiganaji wanaounga mkono serikali na wale wa upinzani walipigana katika mitaa ya Mogadishu baada ya Farmajo kuongeza muda wake kusalia madarakani bila uchaguzi mpya.

Soma pia :Viongozi wa majimbo wataka kumalizwa kwa mgogoro wa kimamlaka Somalia

Mfumo wa uchaguzi wa moja kwa moja

Mgogoro wa kikatiba ulitatuliwa tu wakati rais Farmajo alipobatilisha hatua yake hiyo, waziri mkuu Roble akapanga ratiba ya uchaguzi.

Lakini katika miezi iliyofuata, ushindani mkali kati ya wawili hao ulivuruga tena uchaguzi , na kuwatia hofu waangalizi wa kimataifa. Farmajo na Roble walikubali upya kuzika tofauti zao mnamo mwezi Oktoba, na wakatoa wito kwa pamoja ili mchakato wa uchaguzi uharakishwe.

Somalia haijafanya uchaguzi wa  moja kwa moja yaani mtu mmoja kura moja katika kipindi cha miaka 50 na uchaguzi wake unafuata mfumo tata usio wa moja kwa moja.