1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Nigeria kuwaandama wahusika wa mashambulizi ya msikiti

29 Novemba 2014

Rais Gooluck Jonathan wa Nigeria ameapa kuwasaka wahusika wa mashambulizi ambayo yameuwa takriban watu 120 katika miskiti wa kiongozi wa Kiislamu aliyetowa wito wa kupambana dhidi ya Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1Dx2M
Wataalamu wa kukaguwa mabomu katika eneo la maafa Kano.(28.11.2014).
Wataalamu wa kukaguwa mabomu katika eneo la maafa Kano.(28.11.2014).Picha: Reuters

.Takriban watu wengine 270 wamejeruhiwa wakati washambuliaji wawili wa kujitoa muhanga walipojiripuwa na wengine wenye silaha kuwafyatulia risasi waumini wakati wa sala ya Ijumaa katika Msikiti Mkuu wa Kano ambao ni mji mkubwa kabisa katika eneo linalokaliwa na Waislamu wengi kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa kutoka ofisi ya rais imesema Jumamosi (29.11.2014) Jonathan ameyaamuru mashirika ya usalama kuanzisha uchunguzi kamili na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mawakala hao wa ugaidi wanatiwa nguvuni na kufikishwa mbele ya mahakama.

Taarifa hiyo imesema "Rais anayakinisha kwamba ugaidi wa aina yoyote ile unachukiza na ni tishio lisilohalalika kwa jamii yetu".

Msikiti huo umeshikamana na kasri la Emir wa Kano Muhammad Sanusi wa Pili ambaye pia ni sheikh mkubwa wa Kiislamu anayeshika nafasi ya pili nchini Nigeria ambapo wiki iliopita alitoa wito katika msikiti huo huo akiwahimiza wananchi kuchukuwa silaha kupambana na wapiganaji wa itikadi kali wa kundi la Boko Haram.

Emir huyo alikuwa nje ya nchi wakati wa mashambulizi hayo.Mashambulizi hayo yanaonekana kuwa ni kulipiza kisasi kwa wito wake.

Maiti na damu vimetapakaa

Mmojawapo wa manusura wa mashambulizi hayo Muhammad Inuwa Balarabe amesema kwamba " Ilikuwa ni vifo na damu kutapaka kila mahala.Watu wamelala chini wakiwa wamekufa na wengine wakipiga mayowe ya hofu na maumivu."

Wananachi wakiangalia mwili wa mshambuliaji wa kujitowa muhanga ukiteketea Kano. (28.11.2014)
Wananachi wakiangalia mwili wa mshambuliaji wa kujitowa muhanga ukiteketea Kano. (28.11.2014)Picha: Reuters

Fundi huyo wa nguo huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye alikuwa ameungua vibaya mapajani ameliambia shirika la habari la AFP akiwa kitandani hospitalini kwamba alikuwa ndani ya maeneo ya msikiti huo ambapo mara tu baada ya kuanza kwa sala bomu liliripuka na watu kuanza kushambuliwa kwa risasi.

Jonathan amewataka Wanigeria wasikate tamaa wakati huu wa majaribu makubwa katika historia ya taifa lao bali kuendelea kuwa wamoja kukabiliana na adui yao wa pamoja.

Kuongezeka mashambulizi

Manusura mwengine Maikudi Musa ambaye ndugu yake mmoja ameuwawa kutokana na mashambulizi hayo na kushuhudia mwengine akijeruhiwa vibaya sana amesema mtu hujiuliza watu hawa wanafuata dini gani.

Waasi wa kundi la Boko Haram na kiongozi wao Abubakar Shekawi (katikati).
Waasi wa kundi la Boko Haram na kiongozi wao Abubakar Shekawi (katikati).Picha: picture alliance/AP Photo

Amesema "Huwezi kuhalalisha kushambulia na kuuwa watu wasioweza kujitetea unavyotaka kwa kutumia jina la dini."

Masaa machache tu kabla ya mauaji hayo makubwa ya Kano, bomu linaloshukiwa kutegwa pembezoni mwa barabara karibu na msikiti mwengine ulioko mbali kilomita 600 huko Maiduguri liliteguliwa.

Maiduguri ambapo ndiko kulikoundwa kundi la Boko Haram hapo mwaka 2002 tayari kulikuwa na hali ya wasi wasi baada ya washambuliaji wawili wa kike kusababisha maafa katika soko lililofurika watu hapo Jumanne kwa kuuwa zaidi ya watu 45 waliokuwa wakifanya manunuzi pamoja na wafanya biashara.

Maafa ya watu wengi yanayosababishwa na Boko Haram sio tukio jipya katika uasi wao wa miaka mitano.Kwa jumla zaidi ya watu 13,000 inafikiriwa kuwa wameuawa tangu mwaka 2009.

Kutodhibitika kwa Boko Haram

Kufuatia mashambulizi haya ya karibuni kabisa,mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas ameitaka serikali ya Nigeria kuzidisha hatua za kukabiliana na vitisho vya ugaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuchukuwa hatua za ziada kuwalinda raia.

Mohamed Ibn Chambas mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi.
Mohamed Ibn Chambas mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi.Picha: AP

Gazeti mashuhuri la binafsi la This Day Jumamosi (29.11.2014) lilikuwa na kichwa cha habari kinachosema"Boko Haram bila ya udhibiti limeuwa watu chungu nzima katika msikiti wa Kano."

Mtaalamu wa usalama Ona Ekhomu ameuambia mdahalo wa Televisheni kwamba mashambulizi hayo ya karibuni kabisa yanaonyesha taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika liko vitani.

Amekiambia kipindi cha televisheni ya ndani ya nchi kwamba "Haya ni mauaji makubwa,mauaji ya halaiki.Tuko vitani nchini Nigeria,tuko katika vita vinavyoendelea na hatuvipatii ufumbuzi. Tumetingwa na siasa. "

Wakati eneo la kaskazini mwa Nigeria likiwa limekumbwa na hofu,nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad pia zina wasi wasi kwamba umwagaji damu huo utazagaa na kuingia nchini mwao.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/

Mhariri :Caro Robi