Rais wa mpito aapishwa Tunisia
16 Januari 2011Matangazo
Spika wa zamani wa bunge la Tunisia, Fouad Mebazaa amechukua wadhifa wa rais wa mpito, kufuatia rais wa zamani Zine al Abidine Ben Ali, kukimbilia nchini Saudi Arabia. Baada ya mwezi mzima wa ghasia, kumekuwa na uporaji na milio ya risasi ilisikika katika mji mkuu Tunis, huku wanajeshi wakiwa na vifaru wakifanya doria katika mitaa ya mji huo. Karibu watu 50 wanaripotiwa kuwa wameuwawa katika ghasia zilizotokea katika jela moja. Rais wa mpito Mebazaa, ametoa wito wa kutaka utulivu. Baraza la Katiba la Tunisia, limesema kuwa uchaguzi mpya utafanyika katika muda wa siku 60, licha ya viongozi wa upinzani kusema kuwa muda zaidi unahitajika.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amewataka Watunisia kuanzisha kile alichokiita demokrasia ya kweli na ameongezea kuwa Umoja wa Ulaya pia utaunga mkono kile alichokiita mwanzo mpya. Ufaransa, mshirika wa zamani wa rais aliyeondolewa madarakani, Ben Ali, imetoa wito wa kufanywa uchaguzi huru nchini Tunisia haraka iwezekanavyo. Nae Muammar Gaddafi, kiongozi wa Libya iliyo jirani ya Tunisia, amesema kuwa anasikitishwa na kuanguka kwa Ben Ali kutoka madarakani.