1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Marekani, ziarani Afghanistan.

Halima Nyanza15 Desemba 2008

Rais George W Bush wa Marekani, ameonya kwamba bado kunasafari ndefu kuweza kuleta utulivu nchini Afghanistan. Ametoa onyo hilo leo nchini Afghanistan ambako amefanya ziara ya ghafla.

https://p.dw.com/p/GGKp
Rais George W Bush wa Marekani na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.Picha: AP

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari, ambao pia ulihudhuriwa na Rais wa nchi hiyo, Hamid Karzai, katika makazi yake mjini Kabul, Rais Bush amekiri kuwepo kwa ugumu wa kurudisha amani nchini Afghanistan, ambako wanajeshi wa kigeni wapatao elfu 70, wamekuwa wakipambana na wapiganaji, ambao wameongeza kuwepo kwa ghasia nchini humo, tangu majeshi yanayoongozwa na Marekani kuuondoa utawala wa Taliban mwaka 2001.

Aidha amesema kwa sasa hali ni bora zaidi nchini humo, ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2001.

Kipindi cha mwaka huu, ndicho idadi kubwa ya wanajeshi wa kigeni wameuawa tangu kuangushwa kwa utawala wa Taliban, ambapo kamanda mkuu wa jeshi hilo, Jenerali David McKiernan ametaka kuongezwa kwa wanajeshi wa Marekani, zaidi ya elfu 20 kujaribu kudhibiti hali hiyo.

Kwa Upande wake, Rais Karzai amesema Afghanistan inashukuru kwa msaada iliopata na kuongeza kuwa hangependa watu wake waendelee kuwa mzigo kwa jamii ya kimataifa, katika kutegemea misaada.

Alipoulizwa juu ya uwezekano wa kuondolewa kwa vikosi hivyo vya kigeni nchini humo, Rais Karzai alionesha kwamba sasa sio wakati muafaka kuzungumzia uondoaji wa vikosi hivyo.

Awali Rais Bush alikutana na mamia ya Wanajeshi wa Marekani nchini humo, akiwemo kamanda mkuu wa wanajeshi hao, kabla ya kuelekea Kabul kufanya mazungumzo na Rais Hamid Karzai.

Akizungumza na wanajeshi hao, Rais Bush alionya kuwa kupunguzwa kwa idadi ya wanajeshi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo, kutasababisha kuongezeka kwa ghasia.

Aidha, amekiri kuwa hali ya mambo nchini Afghanistan ni ngumu zaidi, kushinda Iraq.

Ameongeza kuwa Aghanistan ni kubwa kushinda Iraq na kwamba ni masikini na kuna matatizo ya miundo mbinu.

Rais Bush aliwasili nchini Afghanistan, baada ya kutembelea Iraq kwa ziara kama hiyo ya ghafla, ambako alikutana na viongozi wa nchi hiyo, na pia alikiri kuwa vita nchini humo ilikuwa ngumu, lakini amesema ilikuwa ni muhimu vilevile kwa usalama wa Marekani na amani duniani.

Rais Bush na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nuri Al Maliki waliweka saini zao katika mkataba wa amani uliosainiwa mwezi uliopita.

Makubaliano hayo yanaitaka Marekani kuondoa majeshi yake nchini Iraq, ifikapo mwishoni mwa mwaka 2011.

Akizungumzia kuhusu Mkataba huo, Rais Bush amesema unaonesha mwelekeo mzuri katika kufikia siku hiyo ya kihistoria.

Akiwa nchini Iraq Rais Bush pia alikumbana na kisa kimoja baada ya mwandishi mmoja wa Habari alipomtukana na kumrushia viatu, lakini hata hivyo Rais huyo wa Marekani aliona, na kukwepa.

Tukio hilo lilitokea wakati alipokuzwa akizungumza na waandishi wa habari, mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nuri Al Maliki.

Hiyo ni ziara yake ya nne na ya mwisho nchini Iraq tangu alipopeleka kikosi cha jeshi nchini humo na kumtoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Saddam Hussein.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanahoji kuwa ziara ya Rais huyo wa Marekani kwa nchi hizo mbili, huenda ni juhudi za kuimarisha sifa yake kabla ya kuondoka madarakani katika kipindi cha miezi miwili ijayo na kumuachia madaraka ya uongozi, Rais mteule Barack Obama, Januari 20.