Rais wa Ujerumani Steimeier akutana na Biden wa Marekani
6 Oktoba 2023Oktoba 6 kila mwaka ni siku ya ukumbusho wa kuwasili kwa walowezi wa kwanza wa Kijerumani katika jimbo la Philadelphia nchini Marekani waliowasili mnamo mwaka 1683. Ikulu ya Marekani imeitaja siku hii kuwa ndio sababu rasmi ya ziara ya rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier nchini humo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Steinmeier katika wadhifa wake wa urais kukutana na rais Joe Biden. Kiongozi huyo amewahi kwenda Marekani mara kadhaa kama rais wa Ujerumani hapo awali lakini aliiepuka nchi hiyo wakati wa uongozi wa rais wa zamani Donald Trump.
Soma pia:Biden azungumza na washirika kuwahakikishia uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine
Uhusiano kati ya wanasiasa hao wawili ulizingatiwa kuwa ni wa mvutano tangu Steinmeier, akiwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, alipomwita Trump "mhubiri wa chuki" mnamo mwezi Agosti mwaka 2016 wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani. Steinmeier pia aliipinga sera ya Trump ya "Marekani Kwanza" ambayo alisema ilienda kinyume na utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria.
Kwenye ziara yake ya sasa nchini Marekani kiongozi huyo wa Ujerumani na mwenzake wa Marekani wanatarajiwa kusisitiza msimamo wao thabiti ikiwa pamoja na ushirika wa nchi zao mbili katika mfungamano wa kijeshi wa NATO ambapo pamoja na washirika wengine wanashirikiana katika kulinda maadili ya demokrasia na kusisitiza msimamo wa kuendelea kuiunga mkono Ukraine.
Viongozi hao watasisitiza umuhimu wa kuendelea kusimama pamoja na Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi. Ujerumani na Marekani zimeahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine kwa kadri itakavyohitajika.
Rais wa Ujerumani anafanya ziara nchini Marekani wakati ambapo pana mashaka juu ya msimamo wa Marekani katika kuendelea kuiunga mkono Ukraine. Kwa sasa rais wa Marekani Joe Biden anakabiliwa na upinzani wa wabunge wa chama cha Republican juu ya Marekani kuendelea kutoa misaada kwa Ukraine.
Wabunge wahafidhina wa chama cha Republican wanapinga misaada hiyo kwa ajili ya Ukraine wakati ambapo kasi ya kuelekea kwenye uchaguzi wa rais mwaka ujao inapamba moto.
Soma pia: Ulaya yataka Marekani kufikiria upya msaada wake kwa Ukraine
Mpaka sasa Marekani ndiyo inayotoa misaada mikubwa zaidi kwa Ukarine. Hata hivyo maombi ya rais Biden ya kutaka dola bilioni 24 zaidi kwa ajili ya Ukraine hayakujumlishwa katika bajeti ya dharura ya kuipeusha Marekani na baa la kuzifunga shughuli zake.
Hata hivyo balozi wa Marekani kwenye mfungamano wa NATO Julianne Smith, amesema suala hilo litapatiwa ufumbuzi na kwamba rais wa Marekani amesema kuna uwezekao wa kutafutwa njia nyingine ya kutoa msaada kwa Ukraine.
Wakati huo huo rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, katika ziara yake nchini Marekani anatarajiwa kukutana pia na mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA Wlilliam Burns ingawa msemaji wake hakutoa maelezo zaidi kuhusu mkutano huo.