Rais wa Korea Kusini aondolewa madarakani
10 Machi 2017Bunge lilimshitaki Park mwezi Desemba kwa kutumia vibaya madaraka na ufisadi baada ya mamilioni ya watu kuandamana wakimtaka rais huyo ajiuzulu kufuatia kashfa mbalimbali za ufisadi na rushwa. Uamuzi huo uliofikiwa na jopo la majaji wanane wa mahakama ya kikatiba ambao hauwezi kukatiwa rufaa unamaanisha Korea Kusini itafanya uchaguzi katika kipindi cha miezi miwili ijayo kumchagua rais mpya.
Inamaanisha pia Park, mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini humo anakuwa kiongozi wa kwanza kuondolewa madarakani baada ya kushitakiwa na bunge, kupoteza kinga ya rais iliyokuwa ikimlinda dhidi ya kufunguliwa mashitaka. Jaji Mkuu wa mahakama hiyo ya kikatiba Lee Jung Mi amesema vitendo vya Park vilihujumu vibaya sheria na demokrasia.
Urafiki wamchongea
Park mwenye umri wa miaka 65 alikutwa na hatia ya kuvunja sheria kwa kumruhusu rafiki yake Choi Soon Sil kuingilia masuala ya kitaifa na kukiuka sheria kuhusu shughuli za utumishi wa umma. Park anadaiwa kuficha uingiliaji huo uliofanywa na Choi na hata kuwashutumu walioyaibua madai hayo.
Kwon Seong Dong mbunge na mwanachama wa kamati ya bunge ya mashitaka amesema uamuzi huo wa mahakama unathibitisha kuwa kila mtu ni sawa mbele ya sheria, hata rais. Park binti wa kiongozi wa zamani wa kiimla aliyeungwa mkono na jeshi la nchi hiyo aliingia madarakani mwaka 2012 baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa kidemokrasia.
Uamuzi waligawa taifa
Watu wawili wameripotiwa kufariki dunia katika maandamano ya umma baada ya kutangazwa kwa hukumu hiyo. Waziri mkuu wa Korea Kusini ambaye pia ni kaimu rais Hwang Kyo ahn amefanya mkutano na baraza la mawaziri na kutoa wito wa utulivu na uthabiti baada ya hatma iliyomfika Park.
Lakini mfumo wake wa uongozi wa kuonekana kujitenga, kukumbwa na kashfa chungu nzima, na ugumu wa kiuchumi na kijamii ulisababisha umaarufu wake kushuka sana na mamilioni ya Wakorea Kusini waliandamana wakitaka ajiuzulu au aondolewe madarakani.
Kulingana na kura za maoni, karibu asilimia 77 ya raia wa nchi hiyo waliunga mkono kuondolewa madarakani kwa kiongozi huyo. Aliomba radhi mara kadhaa kwa athari za kashfa hizo lakini alikanusha madai yote ya kuwa alifanya makosa alipowasilisha taarifa yake kwa mahakama mwezi uliopita. Swahiba wake wa karibu aliyemuingiza matatani Choi Soon Sil, tayari anakabiliwa na mashitaka.
Marekani imesema inatarajia kuwa na uhusiano mzuri na kiongozi ajaye wa Korea Kusini. Ubalozi wa Marekani nchini humo umesema Korea Kusini itaendelea kuwa mshirika wa karibu na kuongeza wanaheshimu maamuzi ya nchi hiyo.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo