Rais wa Italia aitisha kikao na viongozi wa vyama
3 Mei 2018Mattarella tayari amefanya vikao viwili vya mazungumzo ambavyo vimeshindwa kufikisha mwisho mkwamo wakati juhudi mbili zaidi za upatanishi zilizofanywa na spika wa bunge pia ziligonga mwamba.
"Baada ya miezi miwili, msimamo wa awali wa vyama umebadilika. Hakuna matumaini yalijitokeza kupata serikali, ofisi ya mkuu wa taifa hilo imesema, na kuongeza kwamba rais alitaka kusikia iwapo viongozi wa chama wana mawazo mengine.
Nafasi za Mattarella zinapungua kwa kasi sana na uwezekano wa kurejea katika uchaguzi wakati fulani kati ya sehemu ya mwisho ya mwaka huu na miezi ya mwanzo ya mwaka ujao inaonekana kuzidi kupanda.
Uchaguzi wa taifa Machi 4 ulishuhudia muungano wa siasa za wastani za mrengo wa kulia ukiongozwa na chama kinachopinga wahamiaji cha League ukishinda viti vingi na kile kinachopinga utawala cha 5Star kikitokeza kuwa chama kikuu. Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Democratic PD kilishika nafasi ya tatu.
Hatua kadhaa za kutumia kura ya turufu zimezuwia hadi sasa vyama hivyo kukubaliana juu ya muungano, huku misuguano na kukata tamaa kukiongezeka siku baada ya siku.
Uchaguzi mpya
Kusisitiza hali ya hisia ya kupooza, chama cha PD kilikuwa kiamue baadaye leo Alhamis iwapo kufungua mazungumzo rasmi na chama cha 5Star. Hata hivyo, Mattarella hakutaka kusubiri uamuzi wao kabla ya kutangaza mkutano huo siku ya Jumatatu, ikiwa ni kukiri kwamba chama hicho kilichogawika mno hakitaweza kukubaliana kuhusiana na suala hilo.
Baada ya kufikia uamuzi kama huo, kiongozi wa Nyota 5 wiki hii alitoa wito wa kufanyika uchaguzi mpya mwezi Juni, lakini duru katika ofisi ya rais imeliambia shirika la habari la Reuters jana kuwa kiongozi wa nchi atakataa madai hayo.
Badala yake, Mattarella anataka kuunda serikali ya muda ili kutayarisha bajeti ya mwaka 2019 ambayo itaidhinishwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba.
Iwapo viongozi wa vyama watashindwa kukubaliana na utawala wa aina hiyo , ambao bila shaka utaongozwa na mtu ambaye si mwanasiasa, kwa hiyo uchaguzi ujao utafanyika mwishoni mwa mwaka huu , ama huenda mwezi Oktoba.
Mawaziri wakuu wa mwisho wa Italia waliingia madarakani kutokana na makubaliano ya nyuma ya pazia badala ya ushindi katika masanduku ya kura na juhudi za mara kwa mara kufanyia mageuzi sheria za uchaguzi ambazo zitaruhusu kuundwa haraka kwa serikali zimeshindwa kuleta mfumo wa ushindi.
Mfumo mpya wa uchaguzi
Wakati chama cha Nyota 5 kinataka kurejewa kwa uchaguzi haraka , vyama vingine vimeshauri kufanyakazi kwa pamoja kutengeneza mfumo mpya wa uchaguzi. Hata hivyo , kupata kuungwa mkono kwa makubaliano kama hayo katika hali ya sasa ya kisiasa kunaonekana hakuwezekani.
Wakati uongozi wa siku hadi siku nchini Italia unafanywa na waziri mkuu mlezi Paulo Gentiloni , matarajio ya hivi sasa ya kiuchumi kutoka katika halmashauri ya Ulaya yamesisitiza haja ya kuwapo na serikali kamili ambayo itakuwa tayari kufanya mageuzi.
Utabiri unaonesha kwamba uchumi wa Italia unatarajiwa kukua kwa asilimia 1.5 mwaka huu na kiasi ya asilimia 1.2 tu mwaka ujao ikiwa ni kiwango cha chini kabisa miongoni mwa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman