1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Iran ataka mazungumzo ya kutatua mzozo wa nyuklia kuanza mara moja

7 Agosti 2013

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema yuko tayari kwa mazungumzo ya kuleta tija kuhusu mpango wa nchi hiyo wa kinyukila na kuibua matumaini juu ya uwezekano wa kupigwa hatua baada ya miaka mingi ya mzozo huo

https://p.dw.com/p/19LFz
Picha: Irna

Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari tangu kuapishwa Jumamosi iliyopita,Rouhani amesema hataacha haki za nchi yake kupata nishati ya nyuklia, lakini pia anataka kuondoa hofu zilizonazo nchi za magharibi.

Rouhani anayechukuliwa na mataifa ya magharibi kuwa na msimamo wa wastani amesema anapania kuumaliza mzozo huo na yuko tayari kuingia katika mazungumzo ya uhakika na yenye lengo la kupata muafaka kuhusu suala hilo.

Matumaini ya kuutanzua mzozo huo wa kinyuklia yameongezeka kufuatia ushindi wa Rouhani katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi jana dhidi ya wapinzani wake wenye mitazamo ya kihafidhina.

Kiwanda cha kinyuklia cha Iran
Kiwanda cha kinyuklia cha IranPicha: picture-alliance/AP Photo

Nchi za magharibi na Israel zimesema katika kipindi cha nyuma kuwa zinaamini Iran inajaribu kutengeneza silaha za kinyuklia lakini Iran imekuwa ikisisitiza kwamba mpango wake huo ni kwa matumizi ya amani tu.

Mpango wa kupata nishati hautatupiliwa mbali

Kiongozi huyo wa Iran mwenye umri wa miaka 64 amesema nchi yake haitasitisha mpango wake wa kinyukila ambao amesema utaendelea kuambatana na misingi ya sheria za kimataifa na kuongeza kuwa ni haki ya taifa hilo.

Hata hivyo amesema yuko tayari kwa mazungumzo na ushirikiano bila kupoteza wakati, kukaribia meza ya mazungumzo na upande mwingine kwenye mzozo huo.

Mazungumzo ya mwisho kati ya Iran na Marekani, Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujeruani yalifanyika mwezi Aprili na yalishindwa kusuluhisha mgogoro huo.

Rouhani katika mkutano na mawaziri wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya(2004) kuhusu mpango wa Iran wa nyuklia
Rouhani katika mkutano na mawaziri wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya(2004) kuhusu mpango wa Iran wa nyukliaPicha: AP

Tangu kushinda kwa Rouhani,Marekani imesema iko tayari kushirikiana na nchi hiyo iwapo itakuwa na azma ya dhati kuumaliza mzozo huo kwa njia ya amani.

Pendekezo la mazungumzo lahimizwa

Urusi hapo jana imesema duru mpya ya mazungumzo kati ya iran na nchi hizo zenye nguvu ulimwenguni haipaswi kucheleweshwa na inapaswa kufanyika katikati ya mwezi ujao.

Rouhani ambaye alikuwa mpatanishi wa masuala ya nyuklia wa nchi yake mwaka 2000 bado hajamtaja mpatanishi atakayeiwakilisha Iran katika mazumngumzo hayo mapya.

Akiwa ziarani nchini Italia, Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi inakubaliana kabisa na Rouhani na kushutumu hatua za kuongezea makali vikwazo dhidi ya nchi hiyo na kuongeza kuwa huu si wakati wa masharti bali mazungumzo.

Umoja wa Ulaya umemuandikia barua Rouhani hapo jana na kusema ana jukumu kubwa katika mazungumzo na kwamba umoja huo unatumai kuwepo kwa awamu mpya ya mazungumzo haraka iwezekanayvo.

Rais huyo wa Iran hata hivyo ameionya Marekani kwa kile alichokitaja mtazamo wao kuuma na kupiliza kuhusu suala hilo la kutaka mazungumzo na wakati huo huo kukaza mbinyo kupitia vikwazo dhidi yake ambavyo vimeathiri uchumi wa taifa hilo kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Gakuba Daniel