1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar: Rais wa Iran ahudhuria mkutano wa kilele wa gesi

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
21 Februari 2022

Rais wa Iran Ebrahim Raisi afanya ziara ya kwanza kwenye nchi za Ghuba tangu alipoingia madarakani. Kiongozi huyo anahudhuria mkutano wa kilele masuala ya gesi ambao unatawaliwa na mvutano kati ya Urusi na Ukraine.

https://p.dw.com/p/47MKI
Katar | Ebrahim Raisi trifft Emir Tamim bin Hamad Al Than
Picha: Qatar News Agency/AP/picture alliance

Rais huyo wa Iran na Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, mshirika wa karibu wa Marekani, wanatarajiwa pia kujadili juhudi za kuyafufua makubaliano ya kimataifa yaliyokwama juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema anatarajia safari yake hiyo nchini Qatar itanawirisha uhusiano wa kisiasa na kibiashara kati ya Iran na nchi za Kiarabu za Ghuba.

Rais wa Iran Ebrahim Rais aklikaribishwa mjini Doha na mwenyeji wake Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani.
Rais wa Iran Ebrahim Rais aklikaribishwa mjini Doha na mwenyeji wake Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani. Picha: Qatar News Agency/AP/picture alliance

Mataifa makubwa yanayouza nje gesi asilia hapo siku ya Jumapili yalianza mikutano mjini Doha kujadili jinsi ya kukidhi mahitaji ya dunia yanayoongezeka huku mgogoro wa Ukraine ukizusha hofu barani Ulaya kuhusu usambazaji wa gesi kutoka Urusi.

Wataalamu wa jukwaa la nchi zinazosafirisha gesi nje (GECF) kutoka nchi wanachama 11 walianza mikutano hiyo kabla ya mazungumzo ya ngazi ya mawaziri yanayofanyika leo hii Jumatatu na kisha kufuatiwa na mkutano wa wakuu wa nchi na serikali utakaofanyika Jumanne.

Mkutano huo unatarajiwa kutawaliwa na mivutano inayoongezeka kati ya Urusi na Ukraine hali ambayo imeongeza mahitaji ya gesi na vile vile ongezeko la bei la bidhaa hiyo kwa watumiaji. Huku hofu katika nchi za Ulaya ikiongezeka kwamba Urusi itaivamia Ukraine, bei ya gesi asilia imeongezeka kwa karibu maradufu kulinganisha na bei za mwishoni mwa mwaka 2020.

Muonekano wa angani wa kiwanda cha kusafisha gesi asilia katika bandari, Qatar.
Muonekano wa angani wa kiwanda cha kusafisha gesi asilia katika bandari, Qatar.Picha: imago/Photoshot/Construction Photography

Mataifa ya Ulaya yanatafuta njia mbadala za ugavi wa gesi mbali na Urusi, ambayo inawasilisha asilimia 40 ya gesi katika soko la Ulaya. Nchi hizo za Ulaya sasa zinakodoleea macho kwa kiasi kikubwa Australia na Marekani, ambazo si wanachama wa jukwaa la (GECF), na mwanachama wa jukwaa hilo Qatar, lakini mataifa mengi yanayozalisha gesi yamesema yana uwezo mdogo wa kuziba pengo hilo. Kwa maana nyingine ni kwamba  hayataweza kupeleka kiasi kikubwa cha gesi barani Ulaya ikiwa Urusi, itasitisha usambazaji iwapo itawekewa vikwazo kutokana na mgogoro kati yake na Ukraine katika hatua ambayo itachukuliwa na Urusi kama njia moja wapo ya kulipiza kisasi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Klimentyev/SNA/imago images

Nchi wanachama katika jukwaa la (GECF) ni pamoja na Urusi, Qatar, Iran, Libya, Algeria na Nigeria ambazo kwa pamoja zinachangia zaidi ya asilimia 70 ya hifadhi ya gesi.

Mataifa yanayozalisha gesi yamesisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unahitajika katika nishati hiyo, na kwamba wanahitaji pia uhakika wa kandarasi za muda mrefu ili bara Ulaya liweze kuhakikishiwa usambazaji. Umoja wa Ulaya umepinga kwa muda mrefu mikataba ya miaka 10, 15 hadi 20 iliyotiwa saini na wateja wengine wakuu wa gesi ya Qatar, ambao ni China, Japan na Korea Kusini. Marekani imeiomba Qatar kulisaidia bara la Ulaya kwa kuandaa usambazaji wa dharura iwapo vita vitaripuka nchini Ukraine.

Vyanzo:RTRE/AFP