1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sepp Blatter atakutana na Putin

17 Julai 2015

Rais wa Shirikisho la Kandanda la Kimataifa – FIFA Sepp Blatter atahudhuria droo ya michuano ya kufuzu katika Kombe la Dunia la mwaka wa 2018 mjini St Petersburg mnamo Julai 25.

https://p.dw.com/p/1G0h6
Blatter mit Putin 13.07.2014 in Rio
Picha: picture-alliance/RIA Novosti

Waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko amesema kuwa Blatter amethibitisha kuhudhuria mkutano huo ambao utaamua makundi ya timu zitakazoshiriki katika dimba la dunia nchini Urusi, na huenda pia akakutana na Rais Vladmir Putin.

Maafisa wa Uswisi wamemhamisha nchini Marekani afisa mmoja kati ya saba waliokamatwa kuhusiana na uchunguzi wa rushwa katika shirikisho la FIFA. Mutko amemtetea Rais Blatter ambaye alitangaza kujiuzulu wadhifa wake kufuatia kashfa hiyo ya rushwa amesema "Unaelewa? Ni kama tu kuishutumu FIFA kuwa mchezaji Fulani au kocha alikiuka sheria za barabarani mahali Fulani. Hauwezi kuwa tu mpuuzi. Ikiwa afisa Fulani kutoka shirikisho la CONCACAF ameiba kitu, nini uhusiano wake na FIFA au shirikisho la soka la kimataifa?"

Akizungumzia uamuzi wa karibuni wa shirikisho la kandanda la Urusi kusitisha mkataba wa kocha wa timu ya taifa Fabio Capello, Mutko alimkosoa Muitaliano huyo "Kocha huyu anayeondoka ametuambia tuna wachezaji wa wastani. Tulijua bila yeye kuwa ni wa wastani. Lakini tulimlipa fedha nyingi kufanya jambo na hawa wachezaji wa wastani – hivyo mtu mwenye wasifu wake na kiwango chake angejaribu kufanya kitu. Hiyo ilikuwa motisha yetu. Sasa imetosha, tutakuwa na kocha Mrusi sasa".

Kutimuliwa kwa Capello kumekuja miaka mitatu kabla ya nchi hiyo kuandaa kiynang'anyiro cha Kombe la Dunia. Shirikisho la kandanda la Urusi halijamtaja mrithi wake lakini vyombo vya habari nchini humo vinasema kocha wa CSKA Moscow Leonid Slutski huenda akachukua mikoba ya uongozi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman