Mgogoro bado upo!
4 Septemba 2009Rais wa Benki kuu ya Ulaya, Jean Claude Trichet, amesema kuwa mgogoro wa fedha ulioikumba dunia bado haujamalizika kabisa.
Bwana Trichet amesema hayo leo mjini Frankfurt baada ya tamko la benki la hapo jana kuwa uchumi unaanza kuinuka tena.
Akizungumza baada ya benki Kuu ya Ulaya kuendeleza riba katika kiwango cha kihistoria cha asilimia moja, bwana Trichet amesema leo kuwa mgogoro wa fedha bado ungalipo na kwamba benki kuu ya Ulaya itaendelea kuchukua hatua za kuyaunga mkono mabenki kwa kadri itakavyowezekana.
Wachunguzi wanasema rais huyo wa benki amesema hayo leo kusahihisha tamko la benki yake la hapo jana la kuonesha matumaini juu ya kumalizika kwa mgogoro wa uchumi.
Lakini rais huyo wa benki Kuu ya Ulaya ameeleza kuwa ni mapema mno kusema mgogoro wa fedha umemalizika.
Bwana Trichet alikuwa anazungumza na wataalamu kwenye kongamano lililoandaliwa na taasisi ya mitaala ya fedha kwenye chuo kikuu cha Göthe cha mjini Frankfurt.
Hatahivyo, bwana Trichet ameeleza wazi kwamba mabenki hatimaye yatapaswa kusimama yenyewe tena kwa migumu yao .
Rais huyo wa benki kuu ya Ulaya pia alifafanua juu ya mkakati wa kuanza kufunga breki katika hatua za benki ambazo zimekuwa zinachukuliwa katika kipindi cha miaka 2 iliyopita.
Benki kuu ya Ulaya imepunguza riba kutoka asilimia 4.25 na imetoa mikopo mikubwa kwa mabenki katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Hatahivyo, bwana Trichet amesema benki yake itaacha kutekeleza hatua za kuyasaidia mabenki ikiwa uchumi utarejea katika hali ya kawaida.
Hatua zilizochukuliwa na benki ya Ulaya katika kutoa mikopo zilizisaidia nchi za Ulaya katika kukabiliana na mgogoro wa uchumi, lakini licha ya hatua hizo nchi 16 zinazotumia sarafu ya Euro ziliingia katika mdodoro wa uchumi kwa mara ya kwanza tokea mwaka 1999.
Baada ya kudorora kwa asilimia 0.1 katika robo ya pili mnamo mwaka huu, eneo la nchi zinazotumia sarafu ya Euro lipo njiani kuelekea kwenye ustawi.
Akisisitiza matumaini hayo, mkuregenzi wa shirika la fedha la kimataifa, IMF, Dominique Strauss -Kahn, amesema leo mjini Berlin kwamba uchumi wa dunia unaanza kuinuka tena na kwamba nchi sasa zinapaswa kupanga namna ya kuacha kutekeleza hatua za kufufua uchumi.
Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE.
Mhariri/. Miraji Othman