1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Uhuru Kenyatta atakiwa kufika ICC

20 Septemba 2014

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC Ijumaa (19.09.2014) imemtaka rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufika katika mahakama hiyo kwa madai kwamba serikali yake inazuwia nyaraka zinazotakiwa na mwendesha mashataka.

https://p.dw.com/p/1DG3x
AU-Gipfel in Addis Abeba, Äthiopien, 31.01.2014 Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta anatakiwa mjini The HaguePicha: Reuters

Nyaraka hizo zinatakiwa na mwendesha mashataka kutayarisha kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kenyatta , ambaye anakabiliwa na mashtaka matano katika mahakama ya ICC kuhusiana na madai ya kuhusika kwake katika kupanga ghasia zilizohusiana na uchaguzi mwaka 2007-2008, ameamriwa kufika katika mahakama hiyo Oktoba 8, mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague imesema katika taarifa.

Kenia Prozess gegen William Ruto in Den Haag Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou BensoudaPicha: Reuters

Itakuwa mara ya kwanza Kenyatta kufika katika mahakama hiyo, kwa kuwa amekuwa akisisitiza mara kadhaa kuwa anataka kubakia nchini Kenya kupambana na wanamgambo wa kundi la al-Shabaab wenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda, na kushughulikia masuala ya kitaifa.

Kenyatta anatakiwa kuhudhuria

Mahakama ya ICC imesema majadiliano na Kenyatta , na siku nyingine ya majadiliano siku moja kabla na mwakilishi wa Kenya, yatalenga katika "hali ya ushirikiano kati ya waendesha mashtaka na serikali ya Kenya na masuala yatakayojitokeza katika tamko la upande wa mashitaka la Septemba 5 mwaka 2014."

"Mwakilishi wa serikali ya Kenya anaalikwa kuhudhuria kikao cha kwanza cha kujadili hadhi na rais Kenyatta anatakiwa kuwapo katika kikao cha pili cha kujadili hadhi," taarifa hiyo imesema.

Mwendesha mashitaka Fatou Bensouda amewataka majaji kuahirisha kesi hiyo kabisa, akiwalaumu maafisa wa serikali ya Kenya kwa kuzuwia upatikanaji wa ushahidi muhimu ambao unaweza kuonesha Kenyatta alifadhili ghasia hizo za kikabila za baada ya uchaguzi ambapo watu 1,200 waliuwawa na wengine laki sita wamekimbia makaazi yao.

Kenia Prozess gegen William Ruto in Den Haag
makamu wa rais wa Kenya William Ruto (kulia)akiwa mjini The HaguePicha: Reuters

Bila ya nyaraka hizo , amesema , hakutakuwa na sababu za msingi kumshitaki kiongozi huyo mwenye nguvu katika Afrika mashariki , na kusababisha mawakili wake kwa mara nyingine tena kuomba kesi hiyo itupiliwe mbali.

Nyaraka muhimu zimezuiwa

Kenya imekana madai kuwa imeiwekea ngumu mahakama ya ICC na kuikatalia kutoa nyaraka hizo, ikiwa ni pamoja na nyaraka zinazohusiana na kampuni, taarifa za benki, manunuzi ya ardhi, uhakiki wa kodi, simu zilizopigwa na rekodi za miamala ya fedha za kigeni.

ICC pia imeahirisha tarehe iliyotangazwa hivi karibuni ya ufunguzi , ---Oktoba 7 -- kwa kuwa Kenya mara kadhaa imechelewesha kesi hiyo. Kesi ya hasimu wake ambaye amegeuka kuwa mshirika , makamu wa rais William Ruto, ambaye anakabiliwa na madai kama hayo, ilianza mjini The Hague Septemba 2013.

Mawakili wa wahanga wa ghasia za mwaka 2007-2008 wameilaumu serikali ya Kenya kwa kuchukua hatua za makusudi za kuzuwia kesi hiyo kuendelea," wakati shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeelezea hali ya kukata tamaa kwa wahanga ambao wamejeruhiwa na kupoteza mali wakati wa ghasia hizo.

DW-Interview Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani Raila OdingaPicha: DW/A. Schmidt

Matukio hayo yamechafua heba ya Kenya kama nguzo ya uthabiti katika kanda hiyo mwishoni mwa mwaka 2007 wakati huo kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipomshutumu rais Mwai Kibaki kwa kughushi matokeo ya uchaguzi.

Kile kilichoanza kama ghasia za kisiasa haraka kiligeuka kuwa mauaji ya kikabila ya watu wa kabila la rais Kenyatta , Wakikuyu, ambao nao walianza mashambulizi ya kulipiza kisasi, na kuitumbukiza Kenya katika wimbi baya kabisa la machafuko tangu uhuru mwaka 1963.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri : Bruce Amani