1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Tshisekedi atuma ujumbe Ituru ili kurejesha amani

Sylvia Mwehozi7 Julai 2020

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ametuma ujumbe huko Ituri, ili kujaribu kurejesha amani katika mkoa huo unaokumbwa na mauaji kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3euBm
Symbolbild - Demokratische Republik Kongo Kindersoldaten
Picha: Getty Images/AFP/L. Healing

Miongoni mwa wajumbe wamo waliohudumia vifungo vya miaka kumi jela, baada ya kuongoza uasi mkoani humo. Wajumbe hao wanawataka wanamgambo, waweke silaha chini na kudumisha amani ili kutoa nafasi ya maendeleo ya mkoa huo.

Ujumbe huo kutoka Kinshasa uliwasili mjini Bunia siku ya Ijumaa, miongoni mwa wajumbe kumi na wawili ni viongozi wa zamani wa waasi Matthieu Ngudjolo, Floribert Njabu, Germain Katanga na Pitchou Iribi.

Siku hiyo hiyo ya ijumaa, kulitokea mashambulizi ambapo watu kumi na watatu waliuwawa. Shirika la kiraia la Ituri limesema idadi ya watu waliouwawa mkoani humo tangu mwezi Januari, imefikia zaidi ya elfu moja mia saba tisini (1,790).

Bunia Oskongo UN Truppen 2006
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa DRCPicha: Getty Images

Maelfu ya raia wengine wameyahama makazi yao kutokana na mashambulizi yanayotokea karibu kila siku katika mkoa huo, yanayofanywa na wanamgambo wa shirika la maendeleo ya Kongo, CODECO, ambao wengi wao ni kutoka  kabila la walendu, kwa mujibu wa shirika hilo la kiraia.

Lengo la ujumbe uliotumwa na rais Tshisekedi ni kujaribu kurejesha amani mkoani Ituri, na umetoa mwito kwa wanamgambo waweke silaha chini ili kuchangia katika shughuli za maendeleo, kama anavyoeleza msemaji wa ujumbe huo, Pitchou Iribi.

"Wakati huu Ituri inahitaji amani ili kuwe na maendeleo. Ujumbe wetu ni kuomba wanamgambo wote waweke silaha chini na kupokea mwito wa baba wa taifa. Hayo ili Ituri irejee katika hali kawaida yaani, hali ya amani. Na huo ndiwo ujumbe wetu."

Kumekuwa na mizozo ya kikabila tangu miaka mingi baina ya walendu na wahema katika mkoa huo wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

DR Kongo Präsident Felix Tshiszkedi
Rais wa DRC Felix Tshisekedi alipoitembelea Ituri mwaka 2019Picha: Presidence RDC/Felix Tshiszkedi

Shirika la kiraia licha ya kuwa linahitaji amani irejeshwe mkoani Ituri, linashangaa kuona kwamba ujumbe kutoka Kinshasa unajumuisha wajumbe wa kabila moja tu, jambo lisilo la kuridhisha.

Bwana Dieudonnee Lasso Dhekana, msemaji wa shirika la kiraia la Ituri anashindwa kuelewa kwa nini watu wa kabila nyingine hawakushirikishwa katika ujumbe huo, ili kuchangia uhamasishaji wa amani na kisha kutumaini wajumbe kutoka kabila moja watapokelewa na kukubaliwa na kabila zote. Huyu hapa, Dieudonnee Lasso Dhekana.

"Hatujuwi kwa nini serikali ya Kongo ilipenda kututumia kabila moja tu. Wangelishirikisha hata kabila nyingine zisizohusika na mzozo ulio hapa Ituri. Kwa bahati mbaya, tumetambua ni kabila moja tu ndilo lilikuja."

Wajumbe hao bado wanaendelea na juhudi na kinachotarajiwa na wengi ni amani, ili wakaazi waliyoihama miji yao waweze kurejea na kuanza tena maisha ya kawaida.

Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.